Na Janeth Raphael MichuziTv -Dodoma
Wataalamu wa bajeti Nchini kubadili mwelekeo wa utendaji wao katika usimamizi wa mipango na bajeti za serikali, akisisitiza kuwa wao ndio nguzo kuu ya mafanikio au changamoto katika utekelezaji wa bajeti.
Akizungumza leo Agosti 18,2025 jijini Ddooma wakati wa kikao kazi cha tathmini ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2024/25 na maandalizi ya bajeti ya mwaka 2025/26 Kamishina wa Bajeti, toka Wizara ya Fedha, Meshack Anyingisye, ameeleza kuwa wataalamu hao wanapaswa kuwa dira na msingi imara katika kuhakikisha taasisi zao zinafuata mpango na miongozo iliyowekwa.
“Nyie ndiyo nguzo muhimu katika taasisi zenu. Wewe kama mtaalamu wa bajeti unayo nafasi kubwa ya kusaidia viongozi kusimamia utekelezaji wa mipango kwa mujibu wa malengo yaliyokubaliwa. Usikubali kuwa sehemu ya kuyumbisha mwelekeo,” amesema
Hata hivyo ameonya kuwa baadhi ya wataalamu wameanza kujihusisha zaidi na siasa badala ya kushikilia taaluma yao, jambo ambalo linaathiri utekelezaji wa bajeti na kusababisha miradi mingi kukwama au kutokamilika kwa viwango vinavyotarajiwa.
“Uzoefu unaonyesha kuwa sisi wataalamu tumeanza kutamani nafasi za wanasiasa. Lakini changamoto nyingi tunazokumbana nazo zinatokana na sisi kukosa ujasiri wa kushauri kwa mujibu wa mipango tuliyojiwekea. Tumeanza miradi mipya wakati mingine iliyopo haijafikia hata asilimia 50 ya utekelezaji,” amesisitiza
Kamishna Anyingisye ameweka bayana kuwa hali hiyo inasababisha serikali kuingia kwenye migogoro na wakandarasi kutokana na kuchelewesha malipo ya miradi ambayo haikupangwa ipasavyo kwenye bajeti.
“Matokeo yake serikali inajikuta inalipa fedha nyingi kupitia kesi zilizofunguliwa na wakandarasi, pesa ambazo hazina tija wala ufanisi unaotarajiwa,” ameongeza
Amesisitiza kuwa kikao hicho ni cha kitaalamu, hivyo ni lazima kila mmoja atafakari kwa kina maana ya utekelezaji wa bajeti na matarajio yake, huku akisisitiza umuhimu wa kutumia mafunzo hayo kama nyenzo ya kuimarisha usimamizi wa bajeti katika taasisi zao.
Kwa upande wake Kamishna Msaidizi wa Bajeti, Fundi Makama, amesema kuwa kikao hicho ni sehemu muhimu ya mchakato wa uandaaji wa bajeti ya serikali kwa mwaka ujao wa fedha, pamoja na kufanya tathmini ya utekelezaji wa bajeti iliyomalizika mwezi Juni mwaka huu.
Aidha Makama ameeleza kuwa kikao hicho kimewaleta pamoja wadau kutoka mikoa yote ,Wizara mbalimbali za serikali, na Taasisi nyingine muhimu, kwa lengo la kujadili mafanikio na changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wa bajeti ya mwaka uliopita.
“Kupitia kikao hiki, tunapata nafasi ya kujifunza kutoka kwenye changamoto zilizojitokeza, lakini pia kubaini fursa mpya ambazo bajeti iliyopita imezalisha kwa maendeleo ya taifa,” amesema Makama.
Makama ameaongeza kuwa kikao hicho ni hatua ya awali katika mchakato wa uandaaji wa muongozo wa bajeti, ambao baadaye utafuatiwa na hatua ya maandalizi ya mpango na bajeti kamili ya mwaka mpya wa fedha. Hii ni sehemu muhimu ya kuhakikisha kuwa serikali inapanga kwa ufanisi matumizi ya rasilimali zilizopo ili kufanikisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Katika sehemu ya kwanza ya kikao hicho, washiriki watapewa mafunzo kuhusu matumizi sahihi ya mfumo ulioboreshwa wa uandaaji na usimamizi wa bajeti, ambapo Makama amesisitiza umuhimu wa wataalamu kutumia mfumo huo kikamilifu.
Naye Katibu Tawala Msaidizi Mipango na Uratibu Mkoa wa Geita,Deodatus Kayango, amesema kuwa mchakato wa upangaji wa bajeti ya serikali huanzia katika ngazi ya chini ya utawala, yaani serikali za mitaa, kabla ya kupanda hadi ngazi ya halmashauri, mkoa, na hatimaye kufikia serikali kuu.
Kayango ameeleza kuwa hivi sasa serikali inatumia mifumo ya kidijitali kurahisisha mchakato wa kupanga bajeti, tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma ambapo kulikuwepo na changamoto kubwa za ucheleweshaji na ukosefu wa uwiano wa mipango.
“Tunaanzia ngazi ya chini kwa sababu ndiko zinakotoka mahitaji halisi ya wananchi. Serikali imeweka mfumo madhubuti wa kuhakikisha kila hatua katika upangaji wa bajeti inazingatia vipaumbele vya wananchi,” amesema Kayango.