Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Azam FC, Thabit Zakaria maarufu Zaka Zakazi, amesema maandalizi ya kisaikolojia kwa wachezaji wa Taifa Stars ni jambo la msingi kuelekea mchezo wa robo fainali ya CHAN 2024 dhidi ya Morocco.
Akizungumza leo Jumatano, Agosti 20, 2025, katika Mwananchi X Space iliyoandaliwa na Mwananchi Communications Limited (MCL) yenye mada: Nini kifanyike Taifa Stars kutoboa kwenda nusu fainali?, Zaka alisema changamoto kubwa inayowakabili wachezaji ni shinikizo la hatua hiyo muhimu.
“Kwa hatua waliyofikia, wanahitaji kuandaliwa kisaikolojia kwa sababu ni hatua ngumu na muhimu pia kwetu kama wenyeji wa michuano hii. Hata sisi mashabiki tunatakiwa kuonyesha thamani yetu kwa kuipambania timu,” amesema Zaka.
Ameonya kuwa Morocco ni hatari hasa kwenye mipira ya kutenga (set pieces), hivyo Stars inapaswa kuongeza umakini na kuepuka makosa madogo yanayoweza kuwatoa mchezoni.
“Nilimsikia Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe akisisitiza juu ya kukaba kwa nguvu. Ni kweli tunahitaji hilo, lakini tusisahau wapinzani wetu kutoka Afrika Kaskazini ni wajanja na wanajua kushughulika na mechi ngumu,” ameongeza.