GHANA:MENEJA anayefanya vizuri kwa sasa katika kazi za usimamizi wa wasanii Juma Hamad ‘Jayzow’ ameshinda tuzo ya Meneja Bora mwenye Kipaji Afrika katika tuzo zilizotolewa nchini Ghana juzi.
Akizungumza na SpotiLeo, Jayzow alishukuru kwa kupata tuzo hiyo na kusema ni changamoto kwake kuendelea kufanya kazi nzuri zaidi.
“Nashukuru kwa tuzo hii, kwangu naona ni deni la kuendelea kufanya kazi nzuri zaidi ili kuendelea kudhihirisha uwezo wangu, nawashukuru wote wanaoniunga mkono,” alisema.
“Kutoka mitaani ya Tanzania hadi jukwaa la kimataifa hii ni zawadi ya juhudi, nidhamu na mapenzi kwa sanaa na vipaji vya vijana wetu! Si tu ushindi wangu, ni ushindi wa kila kijana anayepambana, kila msanii niliyesimama naye, na kila ndoto ambayo haikukata tamaa!” alisema.
Jayzow mbali na kusimamia miradi ya wasanii wakubwa, pia amejikita kukuza kizazi kipya cha muziki Tanzania.
Kupitia uzoefu wake katika kung’amua vipaji, kutangaza muziki na uongozi amesaidia kuandaa mazingira salama na ya kibiashara kwa vipaji vipya kujitangaza na kufikia hadhira pana.
Pamoja na muziki wa Tanzania kuendelea kupiga hatua katika mataifa mengi duniani huwezi kuacha kutaja eneo la wasimamizi wa wasanii kwa sababu wanafanya kazi nzuri na kutambulika zaidi nje ya Tanzania.
The post Jayzow apata tuzo Ghana first appeared on SpotiLEO.