DAR ES SALAAM: KLABU ya Yanga imeanza rasmi mchakato wa kuwaongezea mkataba nyota wake wa kikosi cha wanawake, Yanga Princess, ambapo mpaka sasa imetaja kumalizana na mabeki wake mahiri Diana Mnally na Uzoamaka Igwe.
Kwa mujibu wa taarifa za klabu hiyo, Mnally ameongezewa mkataba baada ya kuonesha kiwango cha juu msimu uliopita, akichangia mafanikio ya timu hiyo katika mashindano ya ndani.
Hatua ya Yanga inatajwa kuwa sehemu ya mpango wake wa muda mrefu wa kuimarisha kikosi cha wanawake, ikiwa na lengo la kushindana kwa ubora zaidi kwenye Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania (TWPL).
Yanga Princess bado ina matamanio ya kufanya vizuri zaidi msimu ujao hasa baada ya msimu uliopata kumaliza ligi ya wanawake katika nafasi ya tatu.
Huenda inaanza kuwaongezea wachezaji walionesha kiwango msimu uliopita kisha itangaze usajili mpya tayari kuanza maandalizi ya ligi ya Wanawake.
Makamu wa Rais wa Yanga Arafat Haji aliwahi kusema kuwa anatamani kuona klabu hiyo ikichukua taji la Ligi Kuu Wanawake kwani haijawahi tangu kupanda ligi mwaka juzi.
The post Diana, Uzomaka kimeeleweka Yanga Princess first appeared on SpotiLEO.