LAGOS: MSANII wa muziki wa Hip Hop kutoka Nigeria, Keshinro Ololade anayefahamika zaidi kwa jina la kisanii Lil Kesh, ameripotiwa kushambuliwa kwa kutumia silaha jijini Lagos, usiku wa Jumatano, Agosti 20, 2025.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa vyombo vya habari vya nchini humo, Lil Kesh alivamiwa na kundi la watu wasiojulikana waliokuwa na silaha, na katika harakati za kumpora, alidungwa kisu shingoni na kujeruhiwa vibaya kwenye sikio lake la kushoto, hali iliyosababisha sehemu ya sikio hilo kukatwa.
Madaktari waliingilia kati haraka na kufanikisha upasuaji wa kushona sikio hilo huku wakimpatia matibabu ya dharura kuokoa maisha yake.
Hivi sasa, rapa huyo yupo chini ya uangalizi maalum wa kitabibu na inaelezwa kuwa anaendelea kupona, ingawa taarifa rasmi kuhusu hali yake ya kiafya bado haijatolewa.
Aidha, majambazi hao walimnyang’anya Lil Kesh vito vya thamani kubwa, vinavyokadiriwa kuwa na thamani ya mamilioni ya Naira, kabla ya kutoweka kusikojulikana.
Mpaka sasa, mamlaka za usalama nchini Nigeria hazijatoa tamko lolote rasmi kuhusu tukio hilo, na uongozi wa msanii huyo pia bado haujazungumza na vyombo vya habari.
The post Lil Kesh ashambuliwa kikatili Lagos first appeared on SpotiLEO.