*Dkt. Kilabuko atoa wito kwa timu ya uokoaji kuongeza kasi na juhudi za uokoaji
Shinyanga
Mwenyekiti Tume ya Madini atoa Salamu za pole kwa wahanga na waathirika wa ajali Nyandolwa
Imeelezwa kuwa, jitihada za kuendelea kuokoa maisha baada ya ajali ya mgodi kutokea eneo la Nyandolwa mkoani Shinyanga zinaendelea usiku na mchana ambapo hadi kufikia Leo Agosti 21,2025 mafundi 10 kati ya 25 waliokuwa wamekwama chini ya ardhi wameokolewa, huku wanne wakiwa hai, mmoja kati yao akifariki dunia muda mfupi baada ya kufikishwa hospitalini, na saba wakikutwa wamefariki dunia.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mkoani humo ambapo amethibitisha taarifa hizo na kusema kuwa tukio hilo lilitokea takribani siku 10 zilizopita, likisababisha shughuli za uokoaji kuendelea kwa muda mrefu katika mazingira magumu.
Amesema ajali hiyo ilitokea baada ya ardhi kutitia ghafla na kusababisha kifusi kuporomoka katika mashimo (maduara) matatu tofauti yaliyokuwa yakikarabatiwa na mafundi ndani ya mgodi huo, unaomilikiwa na kikundi cha Wachapakazi chini ya leseni ya uchimbaji mdogo.
“Tunaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali kuhakikisha mafundi waliobaki wanatolewa salama. Hili ni tukio la huzuni kubwa kwa mkoa wetu na Taifa kwa ujumla,” amesema Mhe. Mhita.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Dkt. James Kilabuko, ametoa wito kwa timu ya uokoaji kuongeza kasi na juhudi katika shughuli za uokoaji, akisisitiza kuwa kila sekunde ina maana katika kuokoa maisha ya waliobaki chini ya kifusi.
“Natoa pongezi kwa kikosi kizima cha uokoaji kwa moyo wao wa kujitolea, lakini ni muhimu sasa kuongeza kasi bila kuhatarisha usalama wa waokoaji wenyewe,” amesema Dkt. Kilabuko.
Naye, Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Dkt. Janet Lekashingo, amefika eneo la tukio na kutoa salamu za pole kwa familia za marehemu na wote walioathirika na ajali hiyo. Ametoa rai kwa waokoaji kuendelea kuwa na umakini mkubwa na kutanguliza usalama katika operesheni ya uokoaji.
“Hii ni ajali ya kusikitisha mno. Tume ya Madini inatoa pole kwa familia za wahanga, na tutaendelea kufuatilia kwa karibu kuhakikisha taratibu zote za usalama katika migodi zinasimamiwa ipasavyo ili kuepusha ajali kama hizi siku za usoni,” amesema Dkt. Lekashingo.
Aliongezea kuwa, Timu za uokoaji zinajumuisha maafisa kutoka Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Polisi, Tume ya Madini, Wizara ya Madini, wachimbaji wenzao, Mgodi wa Barrick Bulyanhulu, Serikali ya Mkoa na Wilaya ya Shinyanga, ambao wote wanaendelea kushirikiana kuhakikisha mafundi waliobaki wanatolewa salama.
Hadi sasa, juhudi za uokoaji bado zinaendelea katika eneo hilo la mgodi, huku matumaini yakiwa bado hayajapotea kwa familia na ndugu wa mafundi waliobaki chini ya kifusi. Serikali imeahidi kutoa usaidizi wa karibu kwa waathirika na kuhakikisha uchunguzi wa kina unafanyika kubaini chanzo cha ajali hiyo.