
Yanga SC imeitangaza siku ya Ijumaa ya Septemba 12 2025 kuwa siku rasmi ya kilele cha wiki ya Wananchi. Hii ni siku maalum ambayo hutumiwa kwa ajili ya kutambulisha wachezaji na kikosi kipya mbele ya mashabiki.
Pamoja na utambulisho huo matukio kama burudani za muziki na mechi kali ya soka hunogesha. Hili ni miongoni mwa matamasha makubwa ya michezo Afrika.
Historia ya tamasha hili haiwezi kuwekwa mbali na ile ya Tamasha la watani zao wa Jadi Simba SC, ambao walianzisha Simba Day zaidi ya miaka 10 iliyopita.
Simba SC ilianzisha Tamasha hilo kama sehemu ya malengo ya kupata fedha za usajili na gharama nyingine za uendeshaji wa timu.
Ikumbukwe Muasisi wa tamasha hilo kwa upande wa Simba SC wakati ule alikuwa, Hassan Dalali ambaye alikuwa akihudumu katika nafasi ya mwenyekiti. Siku za awali Tarehe rasmi ya Tamasha ilikuwa ni Agosti 8, ambayo kila mwaka Tanzania pia inaadhimisha sikukuu ya wakulima. Kutokana na mabadiliko ya ratiba kila msimu, siku hiyo nayo imekuwa ikibadilika.
Baada ya timu kuwa na misuli ya uongozi pia, lengo kuu likabadilika kutoka kukusanya fedha mpaka kuwa burudani rasmi. Burudani hii huhusisha utambulisho wa wachezaji na benchi la ufundi. Hii pia inahusisha viongozi kuweka wazi shabaha ya timu kwa msimu husika.