DAR ES SALAAM: BEKI mpya wa kimataifa wa Yanga, Frank Assink, amesema yuko tayari kwa changamoto mpya kunako klabu hiyo baada ya kutambulishwa kujiunga nao jana.
Assink mwenye asili ya Ghana amejiunga na Yanga akitokea Singida Black Stars baada ya kuonekana kuwa na kiwango bora msimu uliopita.
Kupitia ujumbe wake alioutoa kwenye mitandao, ameeleza furaha yake akisema yuko tayari kwa mapambano.
“Nina msisimko kwa safari hii mpya! Najivunia kujiunga na Yanga na niko tayari kukabiliana na changamoto zilizo mbele yangu. Niko tayari kwa safari mpya,”amesema.
Ujio wa Assink unatajwa kuongeza nguvu kwenye safu ya ulinzi ya Yanga, hasa ikizingatiwa klabu hiyo ina malengo ya kuendelea kufanya vizuri katika ligi ya ndani na mashindano ya kimataifa.
Assink alianza taaluma yake ya soka nchini Ghana akiwa katika klabu ya Inter Allies, ambapo alitoa huduma kwa timu hiyo kwenye Ligi Kuu ya Premia ya Ghana. A
Mnamo mwaka 2020, alisajiliwa na klabu ya HB Køge ya Denmark akiwa na mkataba wa miaka minne. Baadaye alicheza kwa mkopo kwenye klabu za FKUM Roskilde nchini Denmark na klabu ya Elite Falcons ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).
Assink alikuwa miongoni mwa wachezaji waliofanikisha Ghana kunyakua ubingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 20 mwaka 2021 uliopigwa Mauritania. Pia, amecheza kwa timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 23 ya Ghana.
The post Frank Assink: Niko tayari kupambana Yanga first appeared on SpotiLEO.