MANCHESTER: MABINGWA wa zamani wa Ligi kuu ya England Manchester City wametangaza kuwa Beki wake Ruben Dias ameongeza mkataba wa kuitumikia klabu hiyo wenyeji wa Uwanja wa Etihad hadi 2029.
Tangu alipowasili Etihad kutoka Benfica mwaka 2020 Beki huyo wa kati mwenye umri wa miaka 28 ameichezea City mechi 223 akibeba mataji 10, ikiwa ni pamoja na mataji matatu ya kihistoria wakati klabu yake ilipotawala soka la Ulaya mwaka 2023.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ureno alitwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa Msimu wa Ligi Kuu ya England msimu wa 2020/21 na Mwanasoka Bora wa Mwaka wa Chama cha Waandishi wa Soka, na alikuwa sehemu muhimu kwenye historia ya Man City ya kuwa timu ya kwanza kushinda mataji manne mfululizo ya EPL mwaka 2024.
“Ninajivunia kuwa sehemu ya Klabu hii kubwa. City ndio ninapotaka kuwa, ulipo mpira wa miguu, kushindania mataji. Nia ya Klabu inalingana kikamilifu na nia yangu na kama mwanasoka hakuna kitu bora zaidi kuliko hicho.” – Taarifa ya Man City imemnukuu Dias.
“Jukumu langu sasa ni kuwa bora zaidi muda wote wa mkataba huu, ili niweze kuifanya vyema kazi yangu katika kusaidia kushindania mataji zaidi.” – aliongeza
Mkurugenzi wa Soka wa Manchester City, Hugo Viana amemsifu Dias kwa bidii na weledi wake kazini akisema mchezaji huyo ni mmoja wa wachezaji wasikivu zaidi kwa Meneja Pep Guardiola na anasikilizwa na wachezaji wenzake.
“Ni kiongozi mzuri katika chumba cha kubadilishia nguo na uwanjani. Ni mmoja wa manahodha wetu, wachezaji wanamsikiliza yeye na Pep na wakufunzi wengine wanapenda kufanya naye kazi. Ni mtaalamu wa hali ya juu. Kila Ruben anapovaa jezi yetu anatoa kila kitu kwa ajili ya beji ya klabu.”. – Viana alisema.
The post Dias aongeza miwili Man City first appeared on SpotiLEO.