NEWCASTLE: MENEJA wa Newcastle United Eddie Howe amesema hajamuona wala kuzungumza na mshambuliaji wake Alexander Isak kwa wiki moja na ameelezea Sakata la usajili wake kama “vita isiyo na mshindi” huku akiahidi kuwa atamjumuisha kikosini kama dili lake litafeli.
Mshambuliaji huyo wa Sweden anataka kujiunga na Liverpool lakini ofa ya pauni milioni 110 ilikataliwa na Newcastle mapema mwezi huu. Suala hilo lilipelekea mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25 kutoa taarifa wiki hii akisema Newcastle walivunja ahadi walizotoa kwake.
Isak aliamini angeruhusiwa kuondoka ikiwa klabu kubwa ingekuja kumnunua kwa ada ya usajili inayofaa lakini Newcastle ilijibu kukanusha taarifa hiyo ya Isak na kumshauri amalize mkataba wake wa miaka mitatu au asubiri ofa nono zaidi kutoka Liverpool.
Mchezaji huyo sasa anafanya mazoezi tofauti na kikosi cha kwanza na alikosa mchezo wa ufunguzi wa Newcastle wa msimu mpya wa Ligi Kuu. Na sasa ni wazi hatakuwa sehemu ya kikosi cha Newcastle kitakachomenyana na Liverpool Jumatatu.
“Ana mkataba na klabu hii. Ni mchezaji wetu. Matamanio yangu ni kwamba angekuwa sehemu ya kikosi chetu Jumatatu usiku, lakini hatacheza, na hiyo inanisikitisha kwa sasa. Lakini asilimia 100 nataka kumuona akiwa amevalia jezi ya Newcastle, ndio akirejea nitamrejesha kikosini.” – Howe alisema katika mkutano wa wanahabari uliotawaliwa na maswali kuhusu Isak.
Howe aliongeza kuwa hana jinsi ya kujua kitakamchotokea mshambuliaji huyo wa zamani wa Real Sociedad kabla ya dirisha la usajili kufungwa Septemba 1 lakini anaona ni bora akasalia Newcastle.
The post “Nitamrudisha Isak kikosini” – Howe first appeared on SpotiLEO.