MANCHESTER: MENEJA wa Manchester City Pep Guardiola amesema huenda watakuwa na mshindi wao wa tuzo ya Ballon d’Or Rodrigo Cascante ‘Rodri’ kikosini watakapoikaribisha Tottenham Hotspur mchana wa Jumamosi. Rodri ambaye Guardiola anatumai atasalia ‘fiti’ baada ya kukosa muda mwingi wa msimu uliopita kutokana na jeraha la goti.
Mhispania huyo alikosa mechi ya kwanza Man City ikipata ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Wolverhampton Wanderers wikendi iliyopita kwakuwa hakuwa fiti kucheza mchezo huo baada ya kupata majeraha ya paja kwenye Kombe la Dunia la Klabu mwezi Julai.
“Namtaka Rodri muda wote, ni hivyo tu, Sina shaka yoyote kuhusu uwezo wake au ubora wake. Bado, hadi sasa, ndiye mchezaji bora zaidi duniani. Utimamu utakuja kwa mazoezi na mechi, wiki baada ya wiki na baada ya hapo, kila kitu kitakuwa sawa” Guardiola aliwaambia wanahabari.
Phil Foden pia anarejea kikosini baada ya kukaa nje dhidi ya Wolves kutokana na jeraha la kifundo cha mguu, huku Guardiola akisema ni Mateo Kovacic, Josko Gvardiol na Savinho tu waliobaki nje kutokana na majeraha.
Alipoulizwa iwapo golikipa mpya James Trafford ataanza tena langoni kufuatia uvumi kwamba Ederson yuko mbioni kutimkia Galatasaray ya Uturuki, Guardiola alikataa kusema chochote
Man City wanavaana na Spurs ambao pia walianza vyema msimu mpya baada kuivuruga Burnley 3-0. Guardiola akisema hana shaka meneja wa kikosi hicho Thomas Frank atatengeneza timu hatari sana.
The post Rodri ‘fiti’ kuwavaa Spurs first appeared on SpotiLEO.