Na Mwandishi Wetu
MKURUGENZI Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Ephraim Mafuru, amewakaribisha rasmi wageni na washiriki wote wa Kikao Kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma (CEOs Forum 2025) kitakachofanyika kuanzia Agosti 23 hadi 26 , 2025 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha AICC, jijini Arusha.
Amesema Arusha si tu kitovu cha mikutano ya kimataifa na lango kuu la vivutio vikubwa kama Serengeti, Ngorongoro, Tarangire, Manyara, Mlima Meru na Mlima Kilimanjaro, bali pia ina vivutio vya kipekee vya ndani ya jiji ambavyo vinastahili kutembelewa na wageni.
Ametumia nafasi hiyo pia kuwaomba washiriki na wageni kuchukua muda kutembelea maeneo maarufu yakiwemo ya Makumbusho ya Arusha Manifesto, Makumbusho ya Elimu Viumbe Hai (Natural History Museum, Clock Tower – kitovu cha nusu ya duniani na Chemka chemchem ya maji moto ya asili
Aidha, amewashauri wageni kuonja ladha ya kipekee ya mlo maarufu wa nyama kwa mromboo, ambao ni sehemu ya utalii wa chakula jijini Arusha.
“Kwa wale wanaopenda utalii wa historia, utalii wa utamaduni na utalii wa vyakula, ninawasihi watenge muda wa kutembelea vivutio hivi wakati wakiwa jijini Arusha. Ni sehemu inayokuza utalii wa ndani na kutoa picha halisi ya utambulisho wa Tanzania,” amesema Mafuru.
Ameongeza kuwa mkutano huu mkubwa unaleta fursa ya kuonyesha urithi na vivutio vya Tanzania, huku ukisisitiza nafasi ya Arusha kama jiji la amani, diplomasia na utalii.