Na Mwandishi Wetu, Morogoro
Mashindano ya Selous Marathon yaliyofanyika leo, Agosti 23, 2025 kwa mara ya saba mkoani Morogoro, yameendelea kuvutia maelfu ya washiriki na mashabiki. Miongoni mwa taasisi zilizong’ara ni Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), ambao wameonesha taswira mpya ya ushiriki wa kitaifa kwenye michezo kama nyenzo ya kukuza utalii na afya ya jamii.
TFS, ikiwa mmoja wa wadhamini wakuu wa mashindano, ilishiriki kupitia watumishi wake 35 waliokimbia kilomita 21, 10 na 5. Kupitia ushiriki huo, taasisi hiyo ilitumia mashindano haya kama darasa la vitendo kuendeleza dhana ya utalii wa michezo, kuhamasisha umuhimu wa uhifadhi wa misitu na kuongeza uelewa wa jamii kuhusu vivutio vya asili vilivyopo nchini.
Akizungumza baada ya kukimbia mbio za kilomita 10, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa TFS, Hussein Msuya, alisema ushiriki huo ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo ya viongozi wa taasisi kuhakikisha michezo inakuwa sehemu ya maisha ya kila mfanyakazi ili kupambana na magonjwa yasiyoambukiza na kuimarisha utendaji.
“Ushiriki wetu Selous Marathon si kwa ajili ya mashindano pekee, bali ni kuthibitisha kwa vitendo dhana ya utalii wa michezo kama kaulimbiu yetu inavuosema “Kimbia ukitalii”. Tumeimarisha afya za watumishi wetu, tumeeneza ujumbe wa uhifadhi, na tumechangia kukuza utalii wa ndani kupitia vivutio vya asili vilivyo chini ya usimamizi wa TFS,” alisema Msuya.
Aliongeza kuwa michezo imeendelea kuthibitisha nafasi yake katika kujenga taifa, akimnukuu Rais Samia Suluhu Hassan ambaye mara kadhaa amesisitiza umuhimu wa michezo kama sekta yenye mchango mkubwa kiuchumi, kijamii na kiafya.
Kwa upande wake, Ofisa Utalii wa TFS, Salome Kivuyo, alisema taasisi hiyo ilijitofautisha kwa washiriki wake kuvaa jezi maalum zilizoandikwa Visit Hululu Waterfalls, tofauti na zile zilizotolewa na waandaaji wa mashindano.
“Tulitumia mbio hizi kama jukwaa la kutangaza moja ya vivutio vyetu vikubwa Maporomoko ya Maji ya Hululu yaliyopo katika Msitu wa Mazingira
Asilia Uluguru, ulio chini ya usimamizi wa TFS. Maporomoko haya ni kivutio cha kipekee chenye maji safi yanayotiririka mwaka mzima, na ni rahisi kufikika kutoka Dar es Salaam kwa barabara au kupitia kituo cha SGR Morogoro,” alisema Salome.
Aliongeza kuwa mbali na mabango makubwa yaliyowekwa kwenye njia za wakimbiaji na viwanjani, vivutio vingine vya TFS kama misitu ya Uluguru, maporomoko ya Choma na chemchemi ya Charagule pia vilipata nafasi ya kutangazwa.
Miongoni mwa washiriki wa mbio hizo, Natasha Mtenga, alisema hakuamini macho yake baada ya kuona mabango ya vivutio vya TFS.
“Mazingira ya Hululu na Choma Waterfalls kama yalivyoonyeshwa yameniweka na shauku kubwa ya kwenda kujionea uhalisia wake. Huu ni utalii wa aina yake ambao kila Mtanzania anapaswa kuupitia,” alisema kwa bashasha.
Salome pia alitumia nafasi hiyo kuwataka wadau wa michezo na utalii kujiandaa kwa mashindano makubwa yajayo Meru Forest Adventure Race 2025 yatakayofanyika katika hifadhi ya Napuru, Arusha, eneo maarufu kwa utalii wa ikolojia.
“Mashindano haya yamekuwa yakikua mwaka hadi mwaka: kuanzia washiriki 300 msimu wa kwanza, 500 msimu wa pili, na mwaka huu tunatarajia zaidi ya washiriki 700. Ni fursa ya kipekee ya kuunganisha michezo na utalii wa misitu yetu,” alisema.
Washiriki wanaweza kujisajili kupitia namba za malipo zilizotolewa na waandaaji (Vodacom -5815522 Quality Sports Promoter), huku maandalizi yakiendelea kwa shoo mbalimbali na zawadi za kuvutia.