NA DENIS MLOWE IRINGA
MGOMBEA ubunge jimbo la Iringa mjini aliyeidhinishwa na Chama Cha Mapinduzi , Fadhili Ngajilo amechukua fomu za uchaguzi kuwania ubunge jimbo hilo na kuwashukuru wajumbe na viongozi ngazi za juu kumpitisha.
Ngajilo ambaye amesotea kwa miaka 15 nafasi ilisindikizwa na mamia ya wanachama wa CCM katika ofisi za msimamizi wa uchaguzi zilizoko Manispaa na kukabidhiwa fomu hiyo.
Fomu hiyo alikabidhiwa na Msimamizi wa Uchaguzi wa jimbo la Iringa Mjini Robert Rumisha katika ofisi za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) zilizopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Iringa akisindikizwa na wagombea udiwani waliopitishwa na watia nia ya ubunge akiwemo Nguvu Chengula.
Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa Ngajilo alisema kuwa wakati wa kuvunja makundi kwa wale watia nia ndio sasa na tujenge kundi kwa ajili ya ushindi wa Ccm.
Ngajilo aliwashukuru waliomsindikiza, wakiwemo baadhi ya waliokuwa watia nia wa ubunge na chama Cha Mapinduzi chini ya uongozi wa Mwenyekiti wa Chama na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Halmashauri Kuu ya CCM kwa kumuamini na kumpa nafasi ya kupeperusha bendera ya chama hicho katika Jimbo la Iringa Mjini.
Ngajilo alisisitiza umuhimu wa mshikamano ndani ya chama kwa kusema:
“Hili si suala la mtu mmoja ni kazi ya pamoja tuvunje makundi yaliyokuwepo na hata Mimi natangaza Sina kundi kundi langu ni CCM tushikamane kama wana-CCM kwa lengo la kuhakikisha ushindi wa kishindo kwa wagombea wetu wote madiwani, wabunge, na hatimaye Rais.”
Fadhili Ngajilo ni miongoni mwa wanachama wa CCM waliokulia kwenye harakati za kisiasa za chama hicho na amejaribu bahati yake ya ubunge mara tatu mfululizo (mwaka 2010, 2015, na 2020) bila mafanikio
Ngajilo ameshika nafasi mbalimbali ndani ya CCM ikiwemo kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) na wakati akijitosa katika mchakato huo alikuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Wazazi wa CCM Mkoa wa Iringa.
Uchaguzi Mkuu unatarajiwa kufanyika tarehe 29 Oktoba 2025, na Ngajilo anaingia kwenye kinyang’anyiro hiki akiwa na baraka kamili kutoka ndani ya chama na ari mpya ya kuwatumikia wananchi wa Iringa Mjini.