Na mwandishi wetu, Hanang’
SHIRIKA lisilo la kiserikali la Water Aid Tanzania limeijengea shule ya msingi Bashang Kata ya Wareta Wilayani Hanang’ Mkoani Manyara, matundu 23 ya vyoo vya wanafunzi, walimu na wenye mahitaji maalum, miundombinu ya kuvuna maji ya mvua ya kudhibiti magonjwa ya mlipuko ikiwemo homa ya matumbo na kipindupindu.
Pia, shirika hilo limezindua ofisi yake Tawi la Hanang’ chini ya mratibu wake Upendo Mtambo kwa lengo la kuwahudumia wakazi wa eneo hilo.
Mkurugenzi mkazi wa shirika la Water Aid Tanzania, CPA Anna Mzinga ameeleza kwamba lengo ni kuhakikisha upatikanaji endelevu wa huduma za maji, vyoo bora na usafi binafsi kwa ajili ya kutunza mazingira ya afya na kuiongezea heshima ya utu kwa kuboresha matokeo ya kufundisha na kujitunza katika jamii.
Ameeleza kwamba Oktoba mwaka 2024 walianza rasmi kuteketeza mradi huo wa mpango wa miezi 12 ili kuimarisha zaidi usafi, mradi umeweza kuwajengea uwezo wahudumu wa afya ngazi ya jamii kutoka Wareta na Laghanga ambao umehamasisha umuhimu wa kuwa na vyoo bora, usafi wa mazingira na usafi binafsi hususani tabia ya unawaji mikono kwa maji tiririka na sabuni.
“Mbinu hii shirikishi imegusa watu 12,505 ya walengwa wa mradi huu na kwa ujumla mradi umegharimu dola za marekani 102,553 sawa na shilingi za kitanzania milioni 262 na wanufaika lengwa wa mradi ni watu 10,050 wakiwemo wanafunzi na walimu 759 ambao wanapata huduma za maji salama, usafi na vifaa vya kunawa mikono shuleni,” amesema.
Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara, Ibrahim Mbogo ambaye alikuwa mgeni rasmi wa hafla hiyo, amewapongeza Water Aid Tanzania kwa kuunga juhudi za Serikali kwa kujenga miundombinu ya maji, vyoo bora na eneo la kunawia mikono katika shule ya msingi Bashang.
“Huu ni udhibittisho tosha wa ufanyaji kazi unaozingatia vipaumbele vya serikali katika kuwahudumia watanzania hususan wanafunzi na walimu wetu kwenye shule hii ya Bashang,” amesema Mbogo.
Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Bashang Yoha na Raphael amesema shule hiyo ina wanafunzi 796 ambao pia ni wanufaika wa mradi huo.
Mwalimu Raphael ameeleza kuwa miundombinu hiyo ni vyumba 23 vya vyoo na ameahidi kuwa watatunza vyema.
Mwakilishi wa The Church of Jesus Christ and later days saint, Denis Mkasa ameeleza kwamba waumini wa kanisa lao lenye miaka karibia 200 wamejichanga na kupata fedha za kujenga miundombinuhiyo ya vyoo.