Moshi.Mgombea ubunge mteule kupitia chama cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la Moshi mjini, Ibrahim Shayo amechukua fomu ya kuwania nafasi ya ubunge kwa mara ya kwanza katika jimbo hilo kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Agosti 23,2025 Halmashauri kuu ya Chama cha Mapinduzi CCM Taifa (INEC), ilitangaza majina ya wagombea ubunge na uwakilishi kupitia chama hicho, kwa majimbo ya Tanzania Bara na Zanzibar, pamoja na viti maalum kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Mfanyabiashara huyo maarufu nchini(Ibraline), amekabidhiwa fomu hiyo leo Jumatatu, Agosti 25, 2025, na Msimamizi wa uchaguzi Manispaa ya Moshi, Sifaeli Kulanga.
Akizungumza mara baada ya kuchukua fomu hiyo, Shayo amekishukuru chama cha Mapinduzi (CCM) kwa imani waliyoonyesha kwake kwa kumteua kupeperusha bendera ya chama hicho katika kinyang’anyiro hicho cha ubunge.
Shayo amesema makundi yote yaliyokuwepo wakati wa mchakato wa kura za maoni ndani ya chama hicho yameungana rasmi kumuunga mkono, hatua aliyosema inaleta mshikamano na umoja ndani ya CCM Jimbo la Moshi Mjini.
Akizungumza, Msimamizi wa uchaguzi wa Jimbo hilo, Sifaeli Kulanga, amesema hadi kufikia leo Jumatatu Agosti 23 majira ya saa 8:15 tayari wagombea 9 kutoka vyama mbalimbali vya siasa wamechukua fomu za kuwania ubunge katika Jimbo la Moshi Mjini.
Amevitaja vyama hivyo ni pamoja CCM, CHAUMA, CCK, CUF, NRA, MAKINI, TLP, SAU, na AAFP.