UONGOZI wa Simba SC umebainisha kuwa sababu kubwa ya Simba Day kufanyika Septemba badala ya Agosti ni ratiba kubana huku wakipanga uzinduzi wa Wiki ya Simba kufanyika mkoano Iringa, wilayani Mafinga.
Ahmed Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba SC amesema kuwa Simba Day ni tamasha kubwa ambalo linazidi kuboreshwa kila siku huku la msimu huu likiwa katika upekee mkubwa.
“Wote mnakumbuka tulitangaza kwamba Septemba 10, 2025 ndio itakuwa Simba Day. Wote mnafahamu mara nyingi Simba Day inafanyika wiki ya kwanza ya mwezi wa nane lakini kutokana na kubanana kwa ratiba na hasa mashindano ya CHAN imefanya imesogea hadi mwezi wa tisa.
“Nayo mwezi wa tisa haikuwa rahisi kupata tarehe sababu ya kubanana kwa ratiba, kuanzia tarehe moja hadi nane ni kalenda ya FIFA, kwa mujibu wa kalenda ya TFF ilionyesha Ngao ya Jamii ilikuwa Septemba 11-14, 2025 hivyo haikuwa na namna nyingine zaidi ya kuiweka Simba Day katikati ya wiki. Vipo vilabu vilihairisha matamasha yao lakini sisi tulisema lazima tufanye.
“Fanya shughuli zako maliza, Septemba 10, 2025 tunakuhitaji uwanja wa Mkapa, hii siku haihitaji sababu, hakikisha unakuja uwanjani. Kwa kawaida Simba Day inakuwa na mfululizo wa matukio ambayo yanaunda Simba Week. Yapo matukio ya kibiashara, yapo ya kijamii, yapo matukio ya aina mbalimbali kunogesha wiki ya Simba.
“Katika msimu huu wa 17 wa Simba Day, utazinduliwa rasmi Agosti 30, 2025, na kama ambavyo tumeanzisha utamaduni wa kufanya uzinduzi wa Wiki ya Simba nje ya jiji la Dar es Salaam basi na mwaka huu itakuwa hivyo. Mwaka jana ilikuwa Morogoro na mwaka huu tutazindua mkoani Iringa kwenye wilaya ya Mafinga.
“Tutaondoka Dar tarehe 30/08/2025 na uzinduzi rasmi utafanyika Agosti 31, 2025 kwenye viwanja vya Mafinga vilivyopo Mafinga Mjini. Kutakuwa na burudani za kutosha na shangwe kubwa vibaya mno.”