Klabu ya Yanga imeanza mikakati ya kuhakikisha inapata ushindi katika mchezo wake wa Ngao ya Jamii dhidi ya watani zao wa jadi, Simba, unaotarajiwa kupigwa, Septemba 16, mwaka huu, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Makamu wa Rais, Arafat Haji, amesema kuwa mipango na mikakati ya mechi hiyo imeshaanza ambapo lengo ni kupata ushindi ili kuendelea kulihifadhi taji hilo.
Alisema kuwa heshima ya Yanga kwa msimu wa 2025/26, itaanza kuwekwa katika mchezo huo.
“Tuna kazi tarehe 16, jamaa walitamani ule mfumo ungeendelea, walitamani ungendelea kuchezwa kwa mfumo wa nusu fainali ili watukimbie tena, lakini wanasema Mungu si Athumani, kawaleta, siku hiyo tutaanza kuweka heshima ya Yanga kwa msimu wa 2025/26,” alisema Haji.
Akaongeza: “Tutakwenda kuhakikisha Ngao ya Jamii inakwenda nyumbani, ibakie Jangwani kwa sababu ni kwao, hivyo ushirikiano wa Wanayanga wote ule uliooneshwa msimu uliopita uongezeke mara dufu msimu huu.”