Na Pamela Mollel,Longido
Wilaya ya Longido imeendelea kupiga hatua kubwa za maendeleo katika sekta mbalimbali chini ya uongozi wa aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo, Steven Kiruswa kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Agosti 26, 2025, Kiruswa alichukua fomu ya kugombea tena ubunge katika Halmashauri ya Longido, akipokelewa kwa shamrashamra na wafuasi wa CCM
Akizungumza baada ya kuchukua fomu, Kiruswa alisema ameendelea kushirikiana na serikali, halmashauri na wadau wa maendeleo katika utekelezaji wa Ilani ya CCM, ikiwemo kuboresha huduma muhimu za kijamii.
Katika sekta ya elimu, amefanikisha ujenzi wa madarasa, mabweni na kuongeza walimu, jambo lililowezesha shule za msingi kufika kila kijiji na sekondari kila kata
Katika sekta ya afya, amesimamia ujenzi wa vituo vya afya pamoja na kuboresha hospitali ya wilaya kwa vifaa tiba na madaktari
Pia amesimamia miradi ya maji kupitia visima na miundombinu ya usambazaji maji safi, sambamba na uboreshaji wa barabara, umeme vijijini na mawasiliano ya simu.
Kiruswa aliwashukuru viongozi wa CCM kwa kumuamini kuendelea kupeperusha bendera ya chama hicho, akiahidi kuendeleza miradi yote ya maendeleo pale aliposhia.
Aidha, aliwataka wafuasi wa CCM kuhakikisha chama hicho kinashinda kwa kishindo katika uchaguzi Mkuu
“Naomba wananchi wa Longido tumchague Rais kwa asilimia 100, Mbunge kwa asilimia 100 na madiwani kwa asilimia 100 ili tuendelee kuipa CCM ushindi wa kishindo,” alisema Kiruswa huku akishangiliwa na umati wa wafuasi wake.