DAR ES SALAAM:KIUNGO wa kimataifa kutoka Nigeria, Precious Christopher, amesema kurejea kwake Yanga Princess ni kama kurudi nyumbani baada ya kutambulishwa rasmi na klabu hiyo jana jijini Dar es Salaam.
Kupitia ukurasa wake wa mitandao ya kijamii, Precious aliandika: “Nyumbani!! Nyumbani!! Nyumbani!! Aya ndugu zangu nimesikiliza na nimerudi nyumban, Mimi siku zote ni Mwananchi,”
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 22 aliwahi kuichezea Yanga Princess kabla ya kusajiliwa na Simba Queens msimu uliopita, ambako alisaini mkataba wa miaka miwili na kuonesha kiwango bora akiwa kiungo mkabaji mwenye nguvu na pasi sahihi.
Msimu uliopita alifunga mabao matatu na kutoa pasi ya bao moja katika Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania (WPL).
Aidha, Precious aliwahi pia kushiriki mashindano ya CAF Women’s Champions League akiwa na Rivers Angels ya Nigeria kabla ya kuhamia Tanzania.
Mbali na Precious, Yanga Princess pia wamemtambulisha kiungo mwingine mpya, Ritticia Nabossa kutoka Uganda, ambaye awali alicheza Fountain Gate Princess kisha kujiunga na Simba Queens.
Nabossa ni miongoni mwa wachezaji tegemeo wa timu ya taifa ya wanawake ya Uganda (Crested Cranes) na amewahi kushinda Ngao ya Jamii ya Wanawake akiwa na Simba.
Usajili wa wachezaji hao wawili unatazamwa kuongeza chachu ya ushindani ndani ya Yanga Princess kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu ya Wanawake.
The post Precious afurahia kurudi Yanga first appeared on SpotiLEO.