DAR ES SALAAM: MSHAMBULIAJI nyota wa Tanzania, Opa Clement, ameanza ukurasa mpya wa maisha yake ya soka baada ya kutangazwa rasmi kujiunga na klabu ya SD Eibar Femenino ya Hispania, inayoshiriki Ligi Kuu ya Wanawake (Liga F).
Taarifa ya klabu hiyo imesema Clement ametua Hispania akitokea FC Juárez ya Mexico na atakuwa sehemu ya safu ya ushambuliaji ya Eibar hadi Juni 2026, akisubiri kufanyiwa vipimo vya afya.
Hatua hii inamfanya kuwa mmoja wa wachezaji wachache wa Tanzania waliowahi kucheza ligi ya wanawake barani Ulaya katika kiwango hicho cha juu.
Opa, alianza kung’ara na klabu ya Simba Queens, akisaidia timu hiyo kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania mara mbili mfululizo (2019/20 na 2020/21). Uhodari wake ulimfungulia milango ya kimataifa baada ya kujiunga na Kayseri Kadın FK nchini Uturuki kwa mkopo, ambako aliendelea kung’ara kwa mabao yake.
Baadaye, alihamia Beşiktaş ya Uturuki ambako alifunga mabao 12 katika mechi 25, kisha akasaini kwa muda na Henan Jianye ya China, alikofunga mabao matano katika mechi 11. Umahiri wake wa kucheka na nyavu ulimpeleka Mexico akiwa mchezaji wa FC Juárez kabla ya Eibar kumvuta Hispania.
Katika ngazi ya kimataifa, Opa ni nahodha wa Twiga Stars na amekuwa mhimili wa timu hiyo katika mashindano mbalimbali.
Aidha, mwaka 2022 alitajwa kwenye kikosi bora cha CAF Women’s Champions League, akionesha kiwango cha juu barani Afrika.
Ujio wake SD Eibar unatarajiwa kuongeza nguvu ya safu ya ushambuliaji ya timu hiyo ambayo inalenga kupanda chati kwenye ligi yenye ushindani mkubwa barani Ulaya.
The post Opa Clement aibukia Hispania, atua SD Eibar first appeared on SpotiLEO.