DAR ES SALAAM: SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu kwa Watu Wenye Ulemavu Tanzania (TAFF) limeomba msaada wa wadau na Watanzania kwa ujumla ili kuhakikisha timu ya taifa ya watu wenye ulemavu, Tembo Warriors, inashiriki michuano ya CECAFA itakayofanyika nchini Burundi kuanzia Septemba 8, mwaka huu.
Makamu wa Rais wa TAFF, Rahel Pallangyo, amesema kuwa tayari Serikali imetoa msaada mkubwa wa usafiri, lakini bado safari haijakamilika kutokana na upungufu wa fedha kwa ajili ya malazi, chakula na posho za wachezaji.
“Tunaomba wadau na Watanzania wote wajitokeze kutusaidia. Tunataka kuhakikisha Tembo Warriors wanashiriki michuano hii na kuipeperusha bendera ya taifa. Tunamuomba mlezi wetu, Rais Samia Suluhu Hassan, ajue kwamba bado tuna safari ndefu,” alisema Pallangyo.
Amefafanua kuwa timu hiyo inatarajiwa kuondoka nchini kati ya Septemba 4 au 5 kuelekea Bujumbura na kila mchango kutoka kwa wadau utakuwa na maana kubwa kwa kikosi hicho.
Ushiriki wa Tembo Warriors unatajwa kuwa zaidi ya michezo pekee, bali pia unaleta heshima kwa taifa na kutoa ujumbe wa kuvunja dhana potofu dhidi ya watu wenye ulemavu.
Aidha, TAFF imetoa namba maalum ya malipo ili kurahisisha michango ya wadau, ambapo mtu yeyote anaweza kuchangia kupitia LIPA NAMBA YA YAS: 6408978, ambapo majina TEMBO WARRIORS NA TEMBO QUEEN yatatokea.
“Tusiiache timu peke yao, kila mchango ni chachu ya uzalendo na nguvu ya kupigania bendera ya Tanzania katika anga la kimataifa,” aliongeza Pallangyo.
Michuano ya CECAFA inatarajiwa kukutanisha timu mbalimbali za Afrika Mashariki na Kati, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mashindano makubwa ya kimataifa kwa watu wenye ulemavu.
The post TAFF yaomba msaada kuwezesha Tembo Warriors CECAFA first appeared on SpotiLEO.