Nashville, Marekani, 28 Agosti 2025
Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo, ameongoza ujumbe wa Tanzania kushiriki Mkutano wa 39 wa Kimataifa wa Mapambano Dhidi ya Dawa za Kulevya (IDEC XXXIX) ulioandaliwa na Mamlaka ya Kudhibiti Dawa za Kulevya ya Marekani (DEA).
Mkutano huo umefanyika kuanzia tarehe 26 hadi 28 Agosti 2025 katika Hoteli ya Renaissance Nashville, jijini Nashville, Tennessee nchini Marekani.
Tukio hili muhimu limewakutanisha viongozi wakuu wa Mamlaka za uthibiti wa dawa za kulevya kutoka mataifa mbalimbali Duniani, likiwa na lengo kuu la kuimarisha mshikamano wa kimataifa katika kupambana na uhalifu wa kimataifa unaohusisha dawa za kulevya.
Mada kuu ya mkutano huu imejikita katika Ushirikiano wa Dunia kwa Mustakabali salama katika kuzibaini changamoto mpya za biashara haramu ya dawa za kulevya, uhalifu wa kimataifa na mbinu za utakatishaji fedha.
Mkutano huo ulienda sambamba na vikao mahususi na warsha maalum za teknolojia ya kisasa ya kukabiliana na dawa za kulevya Duniani.
Tukio hili limeendeleza historia ya IDEC kama jukwaa kuu la kujenga ushirikiano na kubadilishana mbinu kwa vyombo vya kudhibiti dawa za kulevya duniani kote, katika jitihada za kudhibiti mitandao ya kihalifu inafanya biashara na uzalishaji wa dawa za kulevya.
Kupitia ushiriki huu, Tanzania imenufaika kwa kiwango kikubwa, jambo linaloonesha matunda ya jitihada za*Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia.
Moja ya mafanikio makubwa yaliyopatikana ni makubaliano yaliyofikiwa kati ya Tanzania na nchi zinazozalisha kwa wingi kemikali bashirifu ili kudhibiti kemikali hatari zinazotumika katika utengenezaji wa dawa za kulevya.
Pia, Tanzania imepata nafasi ya kujadiliana na nchi zinazozalisha mmea wa Kratom unaotengeneza dawa mpya ya kulevya aina ya Mitragyna Speciosa na kuridhiana njia bora ya kushirikiana kudhibiti dawa hiyo ambayo ambayo hata katika nchi hizo imeorodheshwa kama dawa hatari ya kulevya inayodhibitiwa.
Vilevile, ujumbe wa Tanzania umepata uzoefu kutoka Kwa nchi zinazotengeneza vifaa vya kisasa vya kubaini dawa za kulevya, jambo litakalosaidia kuimarisha udhibiti na usalama katika mipaka.
Pia, mkutano huu umeonesha umuhimu wa kuongeza nguvu katika kudhibiti biashara ya dawa za kulevya inayoendelea kuhamia katika majukwaa ya kidijitali, kwa kushirikisha sekta binafsi.
Pamoja na hayo, nchi washiriki wamejifunza na kukumbushwa umuhimu wa kuwekeza katika upelelezi wa kisayansi kupitia forensic intelligence. Dunia kwa sasa inashuhudia mbinu mpya za kutengeneza dawa za kulevya, ambazo zinapita nje ya mifumo ya kawaida, hali inayotishia ufanisi wa mbinu za zamani za udhibiti. Hii ina maana kwamba, uwekezaji katika teknolojia na sayansi ni muhimu zaidi ili kuendelea kufanikisha vita hii.
Kupitia mkutano huu, Tanzania imepata ushirikiano mpya na nchi mbalimbali pamoja na mashirika ya kimataifa.
Mojawapo ya mafanikio ni makubaliano na shirika kubwa la kimataifa la INL, ambalo limeahidi kushirikiana na DCEA kupambana na biashara ya dawa za kulevya kwa kutumia vifaa vya kisasa hususani kuimarisha Forensic Intelligence.
Pia, kikao muhimu kimefanyika kati ya Kamishna Jenerali Aretas Lyimo na Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti Dawa za Kulevya Nigeria (NDLEA), Brigedia Jenerali Maro, ambapo wamekubaliana kuharakisha makubaliano ya ushirikiano kati ya Tanzania na Nigeria katika vita dhidi ya dawa za kulevya.
Ushiriki wa Tanzania katika mkutano huu unaakisi dhamira ya Taifa katika kulinda usalama wa wananchi na kuimarisha uchumi kupitia mapambano thabiti dhidi ya biashara haramu ya dawa za kulevya kwa kujali UTU na kulinda AFYA za watanzania.
Hatua hii ni mwendelezo wa juhudi za kuhakikisha vijana wa Tanzania wanalindwa dhidi ya athari za dawa za kulevya ili waweze kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya Taifa na kufanikisha malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.