ROME, MADRID: LIGI kuu ya Italia Serie A na LaLiga ya Hispania wamemjibu kamishna wa Umoja wa Ulaya ambaye alitaja mipango yao ya kupeleka mechi za ligi hizo nje ya bara la Ulaya kama “usaliti” kwa mashabiki wa soka wa nchi zao.
Serie A inapanga kupeleka mechi kati ya AC Milan na Como jijini Perth nchini Australia, mapema Februari mwakani huku LaLiga ikitarajia kuhamisha mchezo wa Villarreal dhidi ya Barcelona hadi katika jiji la Miami nchini Marekani mwezi Desemba mwaka huu.
Jana Jumatano Kamishna wa Michezo wa Umoja wa Ulaya Glenn Micallef aliandika kwenye mtandao wa kijamii wa X kuonesha kusikitishwa kwake na hatua hiyo na Kwenda mbali kuiita hatua hio ni Usaliti
“Nimesikitishwa sana na mapendekezo ya kupeleka mechi za ligi za ndani nje ya Ulaya. Kwangu ni wazi Mashindano ya Ulaya lazima yachezwe Ulaya. Soka la Ulaya lazima libaki Ulaya.” Aliandika Glenn.
“Ninaamini kwamba klabu zina deni kubwa la mafanikio yao kwa mashabiki wao wa ndani. Kuhamishia mechi za mashindano yao nje sio ubunifu, ni usaliti.”
Katika taarifa, Serie A imesema “imeshangazwa” na matamshi ya Glenn, na kuongeza kuwa amepuuza uthamani wa kimkakati wa mipango inayolenga kulitangaza soka la Italia kimataifa.
“Kuzungumzia usaliti kwa mechi moja, kati ya mechi 380 za Serie A, ni msimamo mkali kupitiliza na ubinafsi ambao unahatarisha kuzusha taharuki na mijadala kwa watu wengi,” taarifa hiyo ilieleza.
“Kupeleka mechi nje ya bara haimaanishi kuiuza ligi, badala yake ni kuupeleka mchezo wetu kwa watazamaji wapya na kukuza ubora wa soka la Italia. Kwa gharama ndogo kwa mashabiki wa Milan na Como, timu zitafaidika katika suala la umaarufu duniani kote.” Ilieleza taarifa hiyo.
Kwa upande wa Rais wa LaLiga Javier Tebas aliandika kwenye mtandao wa X na kusema kuna “maelfu ya mashabiki, wakiwemo watu wa ulaya” kote ulimwenguni wanastahili kuona timu zao zikicheza moja kwa moja.
“Naelewa kuna wasiwasi, lakini tunahitaji kuweka mambo sawa tunazungumza juu ya mechi moja kati ya 380, za LaLiga” Tebas aliandika kwenye X.
“Nashangaa kwamba hakuna wasiwasi mkubwa kuhusu miradi kama vile ligi ya Ulaya ya Pamoja kati ya NBA na FIBA ambayo kimsingi inavuruga mtindo wa michezo wa Ulaya au kuhusu uharamia, ambao unaharibu mashindano mengi ya kitaaluma.” – aliendelea
Shirikisho la soka la Italia na lile la Hispania tayari wameziruhusu ligi zao kufanya hivyo lakini mechi zote mbili zilizopendekezwa bado zinahitaji idhini kutoka shirikisho la soka Ulaya UEFA na shirikiso la soka Duniani FIFA.
The post LaLiga, Serie A wakerwa na kauli za Glenn first appeared on SpotiLEO.