DAR ES SALAAM: KLABU ya Azam FC inatarajiwa kushuka dimbani kuivaa Vipers SC ya Uganda katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa, ukiwa sehemu ya maandalizi ya msimu mpya wa mashindano ya ndani na kimataifa.
Azam FC iko nchini Rwanda ikimalizia kambi ya maandalizi ya Ligi Kuu na michuano ya kimataifa hivyo, mchezo huo utachezwa kwenye Uwanja wa Kigali Pele.
Mchezo huo unatarajiwa kuwa kipimo muhimu kwa kikosi cha Azam ambacho kimekuwa na maandalizi makali tangu kumalizika kwa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2024/2025, ambapo walimaliza katika nafasi ya tatu.
Azam, maarufu kama Wana Lambalamba, wanatarajiwa kutumia mechi hiyo kupima ubora wa kikosi chao kipya pamoja na mifumo ya kiuchezaji kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa ligi.
Kwa upande wao, Vipers SC ambao ni mabingwa wa Ligi Kuu Uganda, wanakuja na morali ya juu kufuatia mafanikio makubwa katika msimu uliopita. Klabu hiyo imeweka wazi dhamira yake ya kutumia mechi dhidi ya Azam kama maandalizi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika.
Akizungumza kuhusu mchezo huo, Kocha Mkuu wa Azam FC Florent Ibenge amesema mechi hiyo ni sehemu muhimu ya kuangalia uimara wa kikosi chake na kujipima dhidi ya timu bora kutoka ukanda wa Afrika Mashariki.
“Tunakutana na timu bora kutoka Uganda. Tunahitaji kujua tulipo kabla ya mashindano rasmi kuanza. Wachezaji wetu wana ari kubwa, na tunatarajia mchezo wenye ushindani,” amesema.
Rekodi zinaonesha kuwa Azam FC na Vipers SC tayari wamekutana kwenye mechi mbili za kirafiki hapo awali, ambapo Azam waliibuka na ushindi katika zote mbili. Hata hivyo, Vipers wanatarajiwa kuingia uwanjani wakiwa na kikosi kipya chenye wachezaji bora.
Azam FC ikiwa Rwanda imecheza michezo mitatu na kati ya hiyo imeshinda mmoja dhidi ya APR 2-0, sare dhidi ya Polisi 1-1 na kupoteza dhidi ya AS Kigali bao 1-0.
The post Azam FC, Vipers SC kupimana ubavu leo first appeared on SpotiLEO.