DAR ES SALAAM: Timu ya Taifa ya Wanawake ya Kriketi ya Tanzania inatarajiwa kushiriki mashindano ya kufuzu Kombe la Dunia yatakayofanyika nchini Namibia kuanzia kesho hadi Septemba 5, 2025.
Mashindano haya yatazikutanisha timu kutoka nchi 8, zikiwemo Nigeria, Namibia, Kenya, Rwanda, Tanzania, Botswana na Uganda.
Akizungumza wakati akiiaga timu hiyo leo, Ofisa Michezo wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Charles Maguzu, aliwapongeza wachezaji wote waliopata nafasi ya kuiwakilisha Tanzania katika mashindano hayo muhimu ya kimataifa.
“Nawapongeza wote wanaoenda kuiwakilisha nchi kwenye mashindano ya dunia. Benchi la ufundi, naamini mmekusanya kikosi kizuri.
“Mkawasimamie vijana, wapeni moyo na mjenge uzalendo ndani yao. Wanaposhindana wajue kuwa wamebeba taifa la Tanzania nyuma yao,”amesema.
Maguzu amewataka wachezaji hao kuhakikisha wanapambana ili warudi wakiwa wamefuzu.
“Nendeni mkashinde, kwa sababu ushindi ni heshima, muirudishe hapa nyumbani Tanzania.” amesema Maguzu.
Kwa upande wake, nahodha wa timu hiyo, Shufaa Hamza, alieleza imani yake juu ya maandalizi ya timu na dhamira yao ya kupambania ushindi.
“Timu imejiandaa vizuri. Tunaahidi kurudi na ushindi. Tutapambana kadiri tuwezavyo ili kuipeperusha vema bendera ya Tanzania.” amesema Shufaa.
The post Kriketi Wanawake yaangazia Kombe la Dunia first appeared on SpotiLEO.