ISTANBUL: KLABU ya Fenerbahce imetangaza kuachana na meneja wake José Mourinho baada ya klabu hiyo ya Uturuki kushindwa kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya. Kikosi cha Mourinho kilichapwa bao 1-0 na Benfica Jumatano usiku katika mechi ya ‘play-off’ ya kukamilisha timu za UCL.
Katika taarifa iliyotolewa kwenye mtandao wake wa kijamii, klabu hiyo imemshukuru Mourinho kwa juhudi zake katika timu hiyo tangu alipowasili hadi leo na kunamtakia mafanikio katika maisha yake ya baadae.
Meneja huyo wa zamani wa Chelsea, Manchester United na Tottenham anakuwa meneja wa pili mwenye hadhi ya juu nchini Uturuki kutimuliwa siku za karibini baada ya mwenzie Ole Gunnar Solskjaer kutimuliwa na Besiktas chini ya saa moja baada ya kushindwa kufuzu Conference League.
Mourinho alijiunga na Fenerbahce zaidi ya mwaka mmoja uliopita baada ya kuitumikia AS Roma ya Italia na alipokea mapokezi ya kifalme kutoka kwa maelfu ya mashabiki alipofika Istanbul, na hivyo kuibua matarajio ya kumaliza utawala mpya wa Galatasaray.
Kocha huyo mwenye wasifu mkubwa barani Ulaya aliiongoza Fenerbahce katika mechi 62 ambapo alishinda 37, akapoteza 11 na sare 14, na kufanya asilimia yake ya ushindi kuwa 59.68%, idadi yake kubwa zaidi tangu wakati alipokuwa Real Madrid kati ya 2010 na 2013 (71.91%).
The post Mourinho ‘aliwa Kichwa’ Fenerbahce first appeared on SpotiLEO.