DAR ES SALAAM: WAKONGWE wa Ligi Kuu Tanzania bara Simba na Yanga baada ya Ngao ya Jamii Septemba 16, 2025 wanatarajia kukutana tena kwenye Ligi Kuu msimu mpya 2025/26 kwa mara ya kwanza katika Uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es Salaam Desemba 13, 2025, Yanga ikiwa mwenyeji.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa leo na Bodi ya Ligi Kuu, mchezo wa raundi ya pili umepangwa kuchezwa Aprili 4, 2026 Simba akiwa wenyeji.
Aidha, msimu mpya wa Ligi Kuu utaanza Septemba 17 kwa mechi ya KMC dhidi ya Dodoma Jiji Uwanja wa KMC Complex, Mwenge huku Coastal Union ikitarajiwa kucheza na Tanzania Prisons Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Ligi hiyo itafikia tamati Mei 23, 2026.
Katika hatua nyingine, ratiba hiyo inaonesha Yanga inarejea uwanja wa Benjamin Mkapa kama uwanja wake wa nyumbani huku Simba ikibaki KMC Complex, Mwenge vyote vya Dar es Salaam.
Msimu uliopita Simba na Yanga zote zilikuwa zinatumia Uwanja wa KMC kama uwanja wa nyumbani, lakini sasa wekundu wa Msimbazi wamebakia KMC kama ilivyokuwa mwanzo kabla ya Yanga kuukimbia Uwanja wa Chamazi na kumfuata mtani wake wa jadi.
The post Simba, Yanga kazi tena Desemba 13 first appeared on SpotiLEO.