INATAJWA kuwa Simba SC imefanikiwa kumsajili beki wa kati wa Timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars na Klabu ya JKT Tanzania, Wilson Nangu kwa mkataba wa miaka miwili.
Hivyo beki huyo aliyekuwa anatajwa kuwa kwenye rada za Yanga SC huenda msimu mpya wa 2025/26 akawa kwenye uzi wa Simba SC.
Nangu amekuwa bora kwenye timu ya JKT Tanzania kwenye eneo la ulinzi jambo ambalo linatajwa kuwa sababuu ya Simba SC kuisaka saini yake kwa ajili ya kuwa naye kikosini.
Kikosi cha Simba SC kilikuwa kambini Misri tayari Agosti 29 kimerejea kwenye ardhi ya Tanzania kwa maandalizi ya mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara inayotarajiwa kuanza Septemba 17 2025.
Mbali na ligi kuna Simba Day ambayo inatarajiwa kuwa Septemba 10 2025 ambapo kutakuwa na mchezo wa kirafiki dhidi ya Gor Mahia ya Kenya.
Kwa mujibu wa chanzo cha habari kutoka ndani ya Simba, JKT Tanzania imekubali kumuachia nyota kwa sharti la kupewa beki David Kameta na Awesu Awesu kwa mkopo wa mwaka mmoja.
Mbali na Nangu inatajwa kuwa tayari Simba SC imemalizana na kipa namba moja wa JKT Tanzania ambaye alikuwa chaguo la kwanza kwenye mashindano ya CHAN 2024 na timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars Yakoub Seleman ambaye tayari ameshaagwa na timu yake hiyo.