Katika mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia kati ya Uganda na Somalia, tukio la penati limekuwa gumzo kubwa kuliko hata ushindi uliopatikana. Dakika muhimu za mchezo huo zilibeba simulizi ya nidhamu, uongozi na hisia kali baada ya mshambulizi wa Uganda, Steven Mukwala, na mchezaji mwenzake Okello kugombania mpira wa kupiga penati.
Kwa kawaida, timu kubwa huwa na kanuni na majina maalum ya watekelezaji wa penati. Lakini safari hii, hali ilionekana kutofautiana. Wakati refa alipoongeza uamuzi wa penati, Mukwala alijitokeza kwa haraka akitaka kupiga, huku pia Okello naye akionesha dhamira ya kuchukua jukumu hilo. Tukio hilo lilionekana kuzua sintofahamu kwa mashabiki waliokuwa wakifuatilia, wakihisi huenda hali hiyo ingeleta mfarakano ndani ya timu.
Ni katika wakati huo ndipo kapteni wa Cranes, Khalid Aucho, akaonesha mfano wa kweli wa kiongozi uwanjani. Kwa uthabiti na utulivu, alichukua mpira kutoka mikononi mwa Mukwala na kumpatia Okello, akimtambua rasmi kama mpigaji wa penati. Okello hakuwaangusha Waganda, kwani alipiga kwa ustadi na kuipeleka timu yake kifua mbele, huku mashabiki wakilipuka kwa shangwe.
Hata hivyo, kitendo cha Mukwala kutolewa dakika ya 69 kilizua tafsiri nyingi miongoni mwa wachambuzi na mashabiki. Je, ilikuwa ni sababu za kiufundi au ni adhabu ya nidhamu kufuatia “drama ya penati”? Hadi sasa, benchi la ufundi halijatoa kauli rasmi, jambo linaloendelea kuzua mijadala mitaani na mitandaoni.
Kwa upande wa wengi, kitendo cha Aucho kimesifiwa kama mfano wa uongozi bora. Kapteni alihakikisha timu haipasuki kwa sababu ya tamaa binafsi, na badala yake alisimamia nidhamu na mshikamano. Kwa wengine, tukio hili linafunua changamoto za ndani ya kikosi kuhusu uwazi wa majukumu, jambo linalohitaji kusawazishwa mapema ili kuepusha sintofahamu kwenye mechi zijazo.
Kwa ujumla, Uganda ilipata matokeo chanya, lakini tukio hili la penati litabaki kwenye kumbukumbu za mashabiki kama funzo la nidhamu, mshikamano na umuhimu wa uongozi thabiti uwanjani.









