LONDON: NAHODHA wa timu ya taifa ya England Harry Kane amesema kiwango walichoonesha kwenye mechi ya kufuzu kwa Kombe la Dunia waliyoshinda 5-0 dhidi ya Serbia Jumanne kinapaswa kuwa kielelezo cha jinsi wanavyotaka kucheza kufuatia kukosolewa kwa mwanzo mbaya wa kipindi cha kocha Thomas Tuchel.
Kikosi cha Tuchel kilikuwa cha kuvutia zaidi katika mchezo huo wa Jumanne, kikishuhudia wachezaji wake nyota kama, Harry Kane, Noni Madueke, Ezri Konsa, Marcus Rashford na Marc Guehi wote wakifunga bao.
England ilishinda mechi zake zote nne za awali za kufuzu kwenye Kundi K kabla ya mechi hiyo ya mjini Belgrade lakini mbinu za Tuchel na uchaguzi mzuri wa kikosi ulionekana kulipa kufuatia ushindi mnono dhidi ya Andorra, Albania na Latvia.
“Kumekuwa na kelele nyingi huko nje, lakini tunafurahishwa na kile ambacho tumekuwa tukifanya. Si mara zote imekuwa rahisi dhidi ya wapinzani ambao hukaa sana nyuma mara nyingine tunalazimika kuwavunja na kuwa na subira”
“Tulijua usiku wa jana ungekuwa mtihani mkubwa dhidi ya wapinzani bora na wachezaji bora, tulisema tunataka kuonesha tunachoweza kufanya haswa bila mpira na tunapokuwa chini ya shinikizo kubwa na kuifanya mechi iwe ngumu kwao.”
“Unaweza kusema leo ilikuwa kiolezo bora na tutakuwa na michezo migumu kuanzia sasa hadi Kombe la Dunia lakini tutatumia kiwango tulichoonesha mechi hii kama ‘standard’ yetu kuelekea Kombe la Dunia.” – Kane alikiambia kituo cha televisheni cha ITV cha England.
Katika kujiandaa na mechi zijazo za Kundi K, England itamenyana na Wales katika mechi ya kirafiki Oktoba 9 kabla ya kumalizana na Latvia katika mechi ya kufuzu kwa Kombe la Dunia siku tano baadae.
The post Kane ataka England ‘iwake’ first appeared on SpotiLEO.