BERLIN: KOCHA wa Borussia Dortmund Niko Kovac amesema Beki wa klabu hiyo na timu ya taifa Ujerumani Nico Schlotterbeck anahitaji muda zaidi ili kurejea kwenye kikosi baada ya kupona jeraha la goti.
Schlotterbeck alifanyiwa upasuaji miezi mitano iliyopita kutokana na kuchanika kwa mishipa ya ‘meniscus’ kwenye goti lake la kushoto jeraha alilopata mwezi Aprili na licha ya kurudi kwenye mazoezi mepesi ya timu katika siku za hivi karibuni, Kovac anasema bado hayuko tayari kucheza.
“Nico amerejea baada ya miezi mitano na amekuwa akifanya mazoezi mepesi peke yake. Ni mchezaji muhimu, mchezaji wakutumainiwa wa timu ya taifa. Kabla hata hatujafikiria timu ya taifa, lazima awe fiti klabuni na awe na dakika za kucheza mazoezini, kwenye mechi za Bundesliga na Ligi ya Mabingwa”. – Kovac aliuambia mkutano na waandishi wa habari
“Itachukua muda zaidi. Mchezaji wa Bundesliga na hasa beki lazima awe na uwezo wa kukabiliana na mikiki ya washambuliaji katili wa ligi kama anataka kuwa sehemu ya kikosi, na bado hajafikia hapo,” – Kovac aliongeza.
Pengo la Schlotterbeck lilionekana dhahiri katika mechi mbili za kufuzu kwa Kombe la Dunia za taifa lake la Ujerumani lilipochapwa 2-0 na Slovakia kabla ya kuilaza Ireland Kaskazini 3-1.
Dortmund, ambao walikuwa na muda mfupi wa kujiandaa na msimu kutokana na Kombe la Dunia la Klabu, watasafiri hadi Heidenheim kwenye mchezo wa Bundesliga kesho Jumamosi, wakiwa na alama nne kutoka kwenye mechi zao mbili za ligi hadi sasa. Vijana wa Covak pia wataanza kampeni yao ya Ligi ya Mabingwa Septemba 16 dhidi ya Juventus ya Italia.
The post Kovac ampa muda zaidi Schlotterbeck first appeared on SpotiLEO.