CHIȘINĂU: SHIRIKISHO la soka la Moldova (FMF) limetangaza kuwa kocha wa timu ya taifa hilo Serghei Clescenco amejiuzulu kama kocha mkuu kufuatia kufungwa idadi kubwa ya mabao iliyoweka rekodi ya timu ya 11-1 na Norway katika mechi ya kufuzu kwa Kombe la Dunia mapema wiki hii.
Kipigo hicho ndio kipigo kikubwa zaidi kuwahi kutokea kwa timu ya taifa ya Moldova, na kimewaacha mkiani mwa Kundi I wakiwa hawana pointi sifuri katika mechi tano na tofauti ya mabao ya kufungwa 22.
Clescenco, ambaye alichukua majukumu ya kuifunza Moldova mwaka wa 2021, aliiongoza kupanda hadi Ligi C katika UEFA Nations League na alikuwa chupuchupu kufuzu kwa Euro 2024. Lakini, matokeo ya Jumanne yalifuta mema yote ya kocha huyo mwenye miaka 52.
“Katika takriban miaka minne hii tumepitia mengi pamoja, mengine mazuri na kwa mabaya naomba radhi. Kwa muda wote huu nimeona sapoti yenu, kutoka kwa mashabiki, wachezaji, wafanyakazi na shirikisho. Nawashukuru wote kwa imani na kunitia moyo.” – Clescenco alinukuliwa katika taarifa iliyochapishwa kwenye tovuti ya FMF.
The post Kina Haaland waondoka na kocha Moldova first appeared on SpotiLEO.