Morogoro – Watumishi wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) wamekutana kwa siku mbili mkoani Morogoro katika kikao cha Baraza la Wafanyakazi kujadili utekelezaji wa shughuli za Mamlaka kwa mwaka wa fedha 2024/2025 pamoja na kuwasilisha na kuchambua mpango kazi wa mwaka 2025/2026.
Kikao hicho cha siku mbili kilichoanza Septemba 11 hadi 12, 2025 kimeongozwa na Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa TEA, Dkt. Erasmus Kipesha.
Katika kikao hicho, wajumbe walipata fursa ya kupokea taarifa za utekelezaji kutoka kwa vitengo mbalimbali vya Mamlaka, na kutoa maoni na mapendekezo ya namna ya kuboresha utekelezaji wa majukumu kwa ufanisi zaidi.
Akizungumza wakati wa kufungua kikao hicho, Dkt. Kipesha alieleza kuwa Baraza la Wafanyakazi ni jukwaa muhimu linalowawezesha watumishi kushiriki moja kwa moja katika upangaji wa mipango na utekelezaji wa majukumu ya taasisi.
Alisisitiza kuwa ushiriki wa watumishi katika kujadili utekelezaji wa majukumu ya mamlaka na mikakati iliyowekwa kwenye utekelezaji ni msingi wa uwajibikaji, ufanisi na mafanikio ya taasisi kwa ujumla.
“Mkutano huu ni fursa mahsusi ya kujitathmini, kubadilishana mawazo, na kupanga kwa pamoja mikakati ya kuimarisha utendaji wetu ili kufanikisha malengo ya Mamlaka,” alisema Dkt. Kipesha.





Baadhi ya wajumbe wa Baraza la Pili la Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) wakifuatiliauwasilishwaji wa taarifa za utekelezaji katika kikao cha tano cha baraza hilokilichofanyika mjini Morogoro.
