
Mwandishi wa vitabu, mjasiriamali na Mgombea Ubunge Jimbo la Buchosa Eric James Shigongo, ameandika historia mpya kuwa Mtanzania wa kwanza mzungumzaji katika Kongamano la Kimataifa la Wajasiriamali la Norway – Norwegian International Entrepreneur Conference (NIEC) 2025, linalotarajiwa kufanyika tarehe 27 Novemba 2025 kwenye Oslo Concert Hall, Norway.
NIEC ni kongamano kubwa la kimataifa linalowakutanisha wajasiriamali, wawekezaji na viongozi wa fikra kutoka mataifa mbalimbali duniani.
Tangu kuanzishwa kwake mwaka 2011, mkutano huu umekuwa jukwaa muhimu la kubadilishana maarifa na kuhamasisha ujasiriamali wenye tija na athari chanya kwa jamii.
Shigongo atazungumzia mada inayosema: “Creating Wealth in Africa”, akilenga kuonyesha fursa na uwezo mkubwa wa bara la Afrika katika ujenzi wa uchumi endelevu.
Kwa mujibu wa waandaaji tiketi za mkutano huu ni chache na zinapatikana kupitia tovuti yao rasmi www.niec.no.
Kualikwa kwa Eric Shigongo kunachukuliwa kama hatua kubwa ya kutangaza jina la Tanzania kimataifa na ushahidi wa mchango wa Watanzania katika masuala ya ujasiriamali duniani.