Baadhi ya Wakulima wa mahindi wakisubiri kuuza mahindi yao katika kituo cha ununuzi wa zao hilo Kijiji cha Kigonsera Wilaya ya Mbiga Mkoani Ruvuma jana(Picha na Muhidin Amri).
Sehemu ya shehena ya mahindi ya wakulima wa kiiji cha Kigonsera kata ya Kigonsera Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma yakisubiri kupimwa na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula(NFRA)Kanda ya Songea(Picha na Muhidin Amri)
……….
Na Mwandishi Wetu, Mbinga
WAKULIMA wa mahindi katika kata ya Kigonsera Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma,wameishukuru Serikali kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula(NFRA)kanda ya Songea kufungua kituo cha ununuzi wa mahindi kilichosaidia kuuza mahindi yao kwa bei nzuri.
Wakizungumza jana wamesema, kufunguliwa kwa kituo hicho kimekomesha tabia ya baadhi ya wafanyabiashara wanaopita mashambani kuwarubuni wakulima wauze mahindi kwa bei ndogo ya Sh.400 kwa kilo moja na wao kuiuzia Seriali kwa Sh.700.
Said Mohamed alisema,mwaka huu wamefurahishwa na utaratibu wa kununua mahindi uliowekwa kwani wakulima wote wanaopeleka mahindi yanapimwa kwa wakati ikilinganisha na msimu 2023/2024 ambao mkulima alikuwa anakaa kituoni kusubiri kupima mahindi kati ya siku tano hadi saba.
Hata hivyo, ameiomba NFRA kuharakisha malipo baada ya kupima mahindi ili fedha watakazopata watumie kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya wa kilimo 2025/2026 kwa kusafisha mashamba na mahitaji ya shule kwa watoto wao.
Mkulima mwingine Pascal Komba alisema,kufunguliwa kwa soko la mahindi katika kata ya Kigonsera imewezesha wakulima wadogo kupata fursa ya kuuza mahindi kwa bei nzuri na kuipongeza Serikali kwa kuwajali kutokana na kuweka utaratibu mzuri wa kununua mahindi yao.
Alieleza kuwa,hata changamoto ya kukaa kwa muda mrefu kuondoa uchafu ili kupata mahindi safi imepungua sana kwa sababu wakulima wengi wanaanza kuchambua mahindi mashambani kabla ya kufikisha kwenye vituo vya ununuzi.
“Changamoto tuliopata mwaka jana mwaka jana imepungua kwa kiasi kikubwa sana,tunaanza kuchambua mahindi yetu uko mashambani kabla ya kuleta hapa,hii imetusaidia sana kutokaa muda mrefu kwa ajili ya kuchambua, tunaishukuru sana Serikali kwa kutupatia elimu hii na kununua mahindi yetu kwa bei nzuri”alisema.
Naye Msimamizi wa kituo hicho kutoka Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA)Fadhila Amanzi alisema,katika kituo hicho kazi ya ununuzi wa mahindi ya wakulima ilianza rasmi tarehe 24 Julai na wanaendelea kununua mahindi yanayoletwa ambayo ni safi.
Alisema,mwitikio wa wakulima ni mkubwa sana kwani hadi sasa tayari wamenunua zaidi ya tani 17,000 na ununuzi unaendelea na katika msimu wa mwaka huu wakulima wanapeleka mahindi safi ikilinganisha na msimu uliopita ambapo baadhi ya wakulima walishindwa kunufaika na bei ya Serikali baada ya kupeleka mahindi mabovu.
“Nawapongeza sana wakulima wetu kutimia vizuri elimu waliyopewa msimu uliopita kwani mwaka huu wakulima wanaleta mahindi safi hayana uchafu ikilinganisha na msimu uliopita”alisema.