JEAN Ahoua kiungo mshambuliaji namba moja wa Simba SC kwenye mtihani mwingine ndani ya kikosi hicho kinachonolewa na Kocha Mkuu, Fadlu Davids itakuwa Septemba 16 2025.
Ahoua ni namba moja kwenye utengenezaji mipango ndani ya kikosi hicho, msimu wa 2024/25 alitengeneza jumla ya pasi 9 za mabao.
Mbali na kutengeneza pasi hizo 9 za mabao alifunga jumla ya mabao 16 akiwa ni mshambuliaji namba moja kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara inayodhaminiwa na NBC.
Katika pasi na mabao aliyofunga alikwama kufunga mbele ya watani zao wa jadi Yanga SC na alikwama kutengeneza pasi mbele ya watani zake hao jambo ambalo linamfanya awe kwenye mtihani mwingine kujibu maswali aliyokwama msimu uliopita.
Kazi inatarajiwa kuanza Septemba 16 2025 kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii ambapo wababe hawa wawili wanatarajiwa kukutana.
Vita yake kubwa ilikuwa na mwamba Pacome ambaye ni kiungo mshambuliaji wa Yanga SC huyu aliwapa dozi Simba SC walipokutana kwenye mchezo wa funga kazi Uwanja wa Mkapa mzunguko wa pili baada ya kufunga bao moja na kutoa pasi ya bao wakati ubao uliposoma Yanga SC 2-0 Simba SC.
Ni siku moja imebaki kwa watani hawa kukutana uwanjani huku kila mmoja akivutia kwake kuhusu kuanza vema kwa kutwaa taji la Ngao ya Jamii.
Ikumbukwe kwamba kwenye mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Gor Mahia, Ahoua alianza kikosi cha kwanza na alifungua akaunti ya pasi za mabao alipompa Hamza dakika ya 7 na mwisho ubao wa Uwanja wa Mkapa Septemba 10 2025 ulisoma Simba SC 2-0 Gor Mahia.