DAR ES SALAAM:RAIS Dk Samia Suluhu Hassan amempongeza Mwanariadha wa kimataifa kutoka Tanzania Alphonce Simbu baada ya kuibuka Mshindi katika mashindano ya riadha ya Dunia (World Athletics).
Dk samia kupitia kurasa zake za mitandao ya Kijamiii amempongeza kwa kusema “Hongera sana Alphonce Simbu kwa Medali ya Dhahabu ya ushindi wa Mbio Ndefu za Mashindano ya Kimataifa ya Riadha ya Tokyo ndani ya saa 2:09:48 umeandika sehemu ya historia ya Taifa letu”
“Kama nilivyokusihi uliposhika nafasi ya pili kwenye Boston Marathon mwezi Aprili mwaka huu, ushindi wako ni matokeo ya nidhamu yako ya hali ya juu na kujituma kwa bidii kwenye kazi, umekuwa mfano bora kuhusu nguzo hizo mbili za kazi kwa wanariadha na wanamichezo wenzako na hata kwa wasio wanamichezo endelea kuipeperusha vyema na kuiheshimisha bendera ya Taifa letu” amesema Samia.
Simbu ameibuka mshindi katika mashindano ya riadha ya Dunia (World Athletics) mbio za kilomita 42 ambazo zimefanyika Jijini Tokyo nchini Japan na kumshinda Mpinzani wake Raia wa Ujerumani Amanol Petros kwa tofauti ya Sekunde 0.03 na kumfanya apate medali ya kwanza ya dhahabu kwa Tanzania katika mashindano ya dunia ya Tokyo 2025.
The post Dk Samia ampongeza Simbu kwa ushindi Tokyo first appeared on SpotiLEO.