MARRAKECH:KLABU ya Simba SC imepigwa faini ya USD 50,000 (sawa na takribani sh milioni 135 na kuamriwa kucheza bila mashabiki katika mchezo wao ujao wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Gaborone United kutoka Botswana, utakaopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Adhabu hiyo imetolewa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kufuatia tukio la mashabiki wa Simba kuwasha fajiri (fataki/moto) wakati wa mchezo wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita, dhidi ya Al Masry ya Misri uliochezwa kwenye uwanja huo.
Katika mchezo huo uliofanyika April 2025 Simba ilishinda kwa penalti 4-1 kufuatia sare ya mabao 2-2 na wekundu hao wa Msimbazi kufuzu hatua ya nusu fainali.
Katika adhabu hiyo, CAF imeweka marufuku ya mechi mbili za nyumbani kwa Simba ambapo moja ni mchezo dhidi ya Gaborone hatua ya awali utakaochezwa Septemba 28,mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Mechi ya pili imewekwa kwa masharti na itatekelezwa endapo tabia hizo za utovu wa nidhamu zitajirudia.
Hii sio mara ya kwanza Simba kufungiwa msimu uliopita walicheza mchezo dhidi ya CS Constantine bila mashabiki. Ni baada ya vurugu za mashabiki wake katika mchezo dhidi ya CS Sfaxien ambazo zilisababisha kuvunjwa viti 256.
Hatua hii ni pigo kwa Simba SC kwani mashabiki wao wamekuwa nguzo kubwa ya mafanikio ya timu kwenye michezo ya nyumbani, hususan katika mashindano ya kimataifa.
The post Simba kucheza bila mashabiki dhidi ya Gaborone first appeared on SpotiLEO.