Na Mwandishi Wetu, Ngorongoro.
16 Septemba, 2025
Mamlaka ya hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA), kupitia Idara ya Maendeleo ya Jamii na Idara ya huduma za Uhandisi, inaendelea kuimarisha miundombinu ya maji katika vijiji vya Sendui na Irkeepusi vilivyopo tarafa ya Ngorongoro ikiwa ni jitihada za kuboresha upatikanaji wa maji kwa ajili Wanyamapori, mifugo na Wananchi wa vijiji hivyo.
Tathmini iliyofanywa na wataalam wa NCAA itawezesha kufanya ukarabati wa birika la kunyweshea mifugo katika kijiji cha Sendui na kuboresha miundombinu na tenki la kuhifadhia maji lenye ujazo wa lita 140,000 katika shule ya Sekondari ya Nainokanoka ambalo limekuwa manufaa kwa wanafunzi wa shule hiyo na Wananchi kwa Ujumla.
Birika la maji lililopo Kijiji cha Sendui linalohudumia vijiji vya Sendui, Alailelai, na Bulati limefanyiwa tathimini ya ukarabati ambapo timu ya wataalam pia imekagua mradi wa ujenzi wa tenki la maji katika shule ya Sekondari ya Nainokanoka, litakalohudumia kijiji cha Irkeepusi, Shule ya Msingi ya Irkeepusi, Lemala Gate na hoteli zilizopo katika eneo la Lemala.
Pamoja na uboreshaji wa miundombinu ya Maji wataalam wa NCAA kwa kushirikiana na viongozi wa jamii, wanaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu utunzaji wa miundombinu ya maji ili kuendelea kunufaika na miradi hiiyo inayodhaminiwa na Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro.