Wadau wa maendeleo, wasomi na wataalamu kutoka sekta binafsi na umma wamepongeza hatua kubwa zilizopatikana kupitia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, wakibainisha kuwa licha ya changamoto za kiuchumi za kimataifa, Tanzania imeweza kudumisha misingi ya maendeleo. Hata hivyo, walionya kuwa sekta ya kilimo bado ni dhaifu kutokana na utegemezi wa mvua na ukosefu wa viwanda vya zana za kilimo, hivyo kuhitaji uwekezaji mkubwa katika umwagiliaji na miundombinu.
Mjadala huo umeibuka katika Kongamano la Uchumi Jumuishi lililofanyika wiki hii Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kupitia Kigoda cha Profesa cha Mwalimu Julius K. Nyerere, kwa kushirikiana na Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPPC). Washiriki walisisitiza umuhimu wa kujenga uchumi unaogusa moja kwa moja wananchi na kuhimiza ushiriki wa vijana katika sekta za mageuzi.
Mwenyekiti wa kongamano, Profesa Alexander Makulilo, alisema: “Kongamano hili limekuja wakati muafaka, muda mfupi baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuzindua Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 mnamo Julai 17, 2025. Tunapaswa kufahamu kuwa utekelezaji wa dira hii si jukumu la serikali pekee bali la kila Mtanzania kushiriki kwa vitendo.”
Akitoa ufafanuzi zaidi, Ndugu Jordani Matonya alisema dira ya maendeleo imejengwa juu ya misingi ya utawala bora, amani, usalama na mshikamano wa kitaifa. Alibainisha kuwa nguzo kuu tatu za dira hiyo ni uchumi jumuishi na imara, maendeleo ya watu na uhifadhi wa mazingira, huku sekta za mageuzi zikitajwa kuwa kilimo cha umwagiliaji, viwanda, utalii na huduma za kifedha.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPPC), David Kafulila, amesema kuwa ili uchumi uwe wa watu wengi lazima ufuate sekta ambazo zimebeba watu wengi.
“Ili uchumi uwe wa watu wengi, lazima ufuate sekta ambazo zimebeba watu wengi. Ripoti ya siku nyingi kidogo kutoka miaka ya 2008 inasema kwamba ukikuza uchumi kati ya asilimia nane mpaka kumi kwa miaka mitatu mfululizo, utapunguza umasikini kwa asilimia 50,” amesema Kafulila.