DAR ES SALAAM: MSANII wa muziki wa Bongo Fleva, Zuhura Othman maarufu kama Zuchu, ameibuka na malalamiko mazito baada ya kudai kutolipwa malipo ya onyesho alilofanya katika Tamasha la CHAN 2025 lililofanyika jijini Nairobi, Kenya.
Kupitia barua ya wazi aliyoiandikia waandaaji wa tamasha hilo, akiwalenga moja kwa moja Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na kampuni ya Leap Creative Agency, Zuchu amesema licha ya kukamilisha onyesho hilo kwa ubora, hajalipwa fedha zake kama walivyokubaliana.
“Ninaandika kuonyesha wasiwasi na masikitiko yangu kuhusu malipo ambayo bado sijapokea kwa onyesho langu lililofanyika jijini Nairobi, Agosti 30, 2025,” amesema Zuchu, akibainisha kuwa juhudi za timu yake kuwasiliana na maofisa wa Leap Creative Agency hazijazaa matunda.
Ameeleza kuwa malipo hayo yalipaswa kukamilika mara tu baada ya onyesho, lakini hadi sasa hakuna hatua zozote zilizochukuliwa, huku akidai nyaraka za uthibitisho wa malipo alizotumiwa zilionekana kughushiwa. SOMA: Zuchu aitafuta bilioni moja
Kwa mujibu wa Zuchu, aliahirisha baadhi ya maonesho muhimu ili kushiriki kwenye tamasha hilo, hatua ambayo sasa inamfanya ajione kudhalilishwa. “Kama msanii, natarajia kutendewa kwa heshima na haki anayostahili msanii yeyote wa kitaaluma,” amesema na kuongeza kuwa endapo malipo hayo hayatalipwa mara moja, atalazimika kuchukua hatua za kisheria.
Tamasha la CHAN 2025, ambalo ni sehemu ya mashindano ya wachezaji wa ligi za ndani barani Afrika, lilihusisha burudani mbalimbali zikiwemo za muziki, ambapo Zuchu alipewa nafasi ya kipekee ya kuwakilisha Tanzania. Hata hivyo, hadi tunakwenda mitamboni, haijafahamika CAF wala Leap Creative Agency wamesemaje kuhusu tuhuma hizo.
The post Zuchu aibua mapya ya ‘shoo’ ya CHAN 2024 first appeared on SpotiLEO.