Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Mhe. Amina Makilagi, akiwasilisha hotuba yake wakati wa Bonanza la OSHA la Huduma kwa Jamii (OSHA CSR BONANZA 2025) lililofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Nyakabungo Jijini Mwanza akiwa ni Mgeni Rasmi wa Bonanza hilo. Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Mhe. Amina Makilagi na Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda wakimkabidhi Mkuu wa Chuo cha Ufundi cha Mirongo vifaa mbalimbali vya msaada vilivyotolewa na OSHA kukiwezesha chuo hicho. Vifaa vilivyotolewa ni pamoja na kompyuta, makoti ya usalama na vifaa vya michezo.
Na Fredy Mgunda, Kwanza.
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Mheshimiwa Amina Makilagi, amewataka waajiri na wafanyakazi kote nchini kuitekeleza kikamilifu Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi Na. 5 ya mwaka 2003 ili kupunguza au kuondoa kabisa ajali na magonjwa yanayotokana na mazingira duni ya kazi.
Mheshimiwa Makilagi alitoa wito huo jana wakati wa Bonanza la OSHA la Huduma kwa Jamii (OSHA CSR Bonanza 2025) lililofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Nyakabungo, Wilaya ya Nyamagana, Jijini Mwanza. Bonanza hilo lilihusisha shughuli mbalimbali za kijamii na michezo kwa lengo la kuimarisha mshikamano kati ya OSHA na jamii inayohudumiwa, pamoja na kutoa msaada kwa wanafunzi wa Chuo cha Ufundi Mirongo, wakiwemo wenye ulemavu.
Katika tukio hilo, OSHA ilikabidhi vifaa mbalimbali kwa Chuo cha Ufundi Mirongo, vikiwemo kompyuta, vifaa kinga vya usalama kazini, pamoja na vifaa vya michezo kama mipira na jezi za michezo.
Akizungumza kama Mgeni Rasmi, Mheshimiwa Makilagi aliipongeza OSHA kwa juhudi zake za kuhakikisha mazingira salama na yenye afya sehemu za kazi na kuonesha moyo wa huruma kwa makundi maalum katika jamii.
“Nitoe rai kwa waajiri na wafanyakazi nchini kuisoma na kuitekeleza Sheria Na. 5 ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ya mwaka 2003. Sheria hii ikitekelezwa ipasavyo, maeneo ya kazi yatakuwa salama, bila ajali wala magonjwa, hivyo kuongeza tija kazini,” alisema Mkuu wa Wilaya Makilagi.
Aidha, aliihakikishia OSHA ushirikiano wa Halmashauri na Ofisi yake katika kusimamia usajili na ukaguzi wa maeneo ya kazi, sambamba na kutoa ushauri wa kitaalamu juu ya maboresho ya mazingira ya kazi.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, alisema Bonanza hilo ni sehemu ya mpango wa taasisi hiyo wa kurudisha kwa jamii (Corporate Social Responsibility) na kwamba msaada uliotolewa kwa Chuo cha Mirongo umetokana na tathmini iliyofanywa na wataalam wa OSHA baada ya kutembelea chuo hicho.
“Tunaamini kuwa kwa kusaidia vyuo vya ufundi kama Mirongo, tunachangia kwa kiasi kikubwa maandalizi ya wataalamu wa baadaye katika fani muhimu za kiufundi na kazi,” alisema Bi. Mwenda.
Kaimu Mkuu wa Chuo cha Mirongo, Bi. Herieth Richard, pamoja na mwanafunzi wa fani ya ushonaji, Bi. Aneth Augustino, waliishukuru OSHA kwa msaada huo ambao wamesema umeongeza ari ya kujifunza na kushiriki katika shughuli za kijamii.
Bonanza hilo lilihusisha michezo ya mpira wa miguu, mpira wa pete, riadha, na michezo ya jadi kama kukimbia kwenye magunia, kukimbia na ndimu kwenye kijiko, rede na kukamata kuku. Washiriki walitoka OSHA na vyuo vya Ufundi vya Mirongo, Nyakato na Kisesa.
Chuo cha Ufundi Mirongo kinamilikiwa na Serikali chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), na hutoa mafunzo ya umeme, useremala, ushonaji na uchomeleaji kwa vijana wakiwemo wenye mahitaji maalum.