LONDON: WASHIKA mitutu wa London Arsenal wametangaza kuondoka ghafla kwa makamu mwenyekiti Tim Lewis kama sehemu ya mabadiliko makubwa ya bodi ya Klabu hiyo ili kuingiza fikra na nguvu mpya katika harakati zake za kusaka mataji.
Arsenal haijashinda taji loyote kubwa tangu mwaka 2020 huku ikitumia takriban pauni milioni 250 (TZS billioni 831.75) katika dirisha la hili la usajili kununua wachezaji wapya, wakiwemo Viktor Gyokeres, Eberechi Eze na Martin Zubimendi, ili kuimarisha kikosi.
Lewis mwenye umri wa miaka 62 alikua mtu muhimu klabuni hapo akishirikiana na meneja Mikel Arteta na mkurugenzi wa michezo Andrea Berta katika kusimamia matumizi ya fedha hizo zilizolenga kuipa makali ambayo yataiwezesha Arsenal kutwaa taji.
Lewis amekuwa mshauri wa kampuni inayomiliki Arsenal ya Kroenke Sports & Entertainment (KSE), tangu mwaka 2007 na alikuwa makamu mwenyekiti kwa miaka miwili na nusu iliyopita, baada ya kujiunga na bodi hiyo mwaka 2020.
Katika mabadiliko hayo, mkurugenzi mkuu Richard Garlick amechukua nafasi ya Mtendaji Mkuu, huku wawakilishi wa kampuni ya KSE Kelly Blaha, Otto Maly, na mtayarishaji na mwongozaji wa filamu Ben Winston wakiingia kwenye bodi kama wakurugenzi watendaji wasaidizi.
Mwenyekiti mwenza wa Arsenal Josh Kroenke amemshukuru Lewis kwa kubeba jukumu muhimu la kuhakikisha timu hiyo iko katika nafasi nzuri ya kuendeleza azma yao ya kushinda mataji makubwa.
“Kwa kuzingatia nia yetu ya kusonga mbele daima, tutaimarisha bodi yetu kwa kuongeza watu wa taaluma mbalimbali ambao wataleta uzoefu mkubwa kwa klabu. Watu wanaoijua na kuipenda Arsenal, ambao wataleta ujuzi na utaalamu tofauti huku tukiongeza fikra na nguvu mpya kutusaidia sote kufikia malengo yetu.” – Kroenke alisema.
The post Arsenal ‘yafagia’ bodi ya klabu first appeared on SpotiLEO.