Mwenyekiti wa Chama cha Wahasibu Wanawake Tanzania (TAWCA) CPA. Mary Mabiti akimkabidhi jana Mkuu wa Kitengo cha Fedha na Uhasibu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) CPA. Ashura Ally tuzo ya shukrani ya utoaji wa huduma za upimaji wa magonjwa ya moyo kwa wanachama wa chama hicho waliohudhuria mkutano wa TAWCA unaofanyika jijini Arusha. Katika mkutano huo JKCI ilitoa bila malipo huduma ya upimaji wa magonjwa ya moyo kwa wanachama 125.
Mkuu wa Kitengo cha Fedha na Uhasibu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) CPA. Ashura Ally akigawa vipeperushi vya kutoa elimu ya magonjwa ya moyo jana kwa wanachama wa Chama cha Wahasibu Wanawake Tanzania (TAWCA) waliofika katika banda la JKCI kwaajili ya kupata huduma za upimaji wa magonjwa ya moyo inayotolewa katika mkutano wa TAWCA jijini Arusha.
Mhasibu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Edna Sanga akimweleza huduma zinazotolewa na JKCI mwanachama wa Chama cha Wahasibu Wanawake Tanzania (TAWCA) aliyefika katika banda la taasisi hiyo jana kwaajili ya kupata huduma za uchunguzi wa magonjwa ya moyo zinazotolewa na wataalamu wa taasisi hiyo katika mkutano wa TAWCA unaofanyika jijini Arusha.
Afisa Lishe wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Neema Matemba akitoa elimu ya lishe bora kwa mwanachama wa Chama cha Wahasibu Wanawake Tanzania (TAWCA) aliyeshiriki mkutano wa chama hicho unaofanyika jijini Arusha. Katika mkutano huo JKCI ilitoa bila malipo huduma ya upimaji wa magonjwa ya moyo kwa wanachama 125. (Picha na JKCI)
Na Mwandishi Maalumu – Arusha
19/9/2025 Wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wamefanya upimaji wa magonjwa ya moyo kwa wanachama 125 wa Chama cha Wahasibu Wanawake Tanzania (TAWCA) wanaoshiriki mkutano wa chama hicho unaofanyika jijini Arusha.
Mbali na upimaji huo unaofanyika bila malipo JKCI pia ilitoa elimu kuhusu namna ya kujikinga na magonjwa ya moyo, ulaji wa lishe bora na matumizi sahihi ya dawa za moyo kwa wagonjwa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo na Mkuu wa Kitengo cha Vipimo vya Moyo wa JKCI, Dkt. Engerasia Kifai alisema mwitikio umekuwa mkubwa jambo linaloonyesha wananchi wengi sasa hivi wanaelewa umuhimu wa kupima afya zao mara kwa mara.
“Tumewafanya vipimo vya sukari, shinikizo la damu, urefu na uzito wa mwili, pamoja na vipimo vya kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi na mfumo wa umeme wa moyo (ECG). Tunafurahi kuona watu wamejitokeza kwa wingi, hii ni hatua muhimu katika kujikinga na magonjwa ya moyo”.
“Kati ya watu 125 tuliowafanyia vipimo sita tumewaanzishia dawa za shinikizo la juu la damu na wanne ambao walikuwa wanashida ya moyo tumewabadilishia dawa za kutumia na kuwapa dawa ambao zinaendana na matatizo waliyonayo ambazo naamini zitawasaidia”, alisema Dkt. Kifai.
Dkt. Kifai aliwaomba wananchi kujitokeza kwa wingi pale watakaposikia taasisi hiyo inafanya upimaji wa magonjwa ya moyo kwa wananchi kwani huduma hiyo inatolewa bila malipo ikiwa na lengo la kusogeza kwa karibu huduma za kibingwa za matibabu ya moyo kwa wananchi.
“Wiki hii na wiki ijayo kuna wataalamu wenzetu wanafanya upimaji katika maonesho ya madini yanayofanyika mkoani Geita, na katika kuadhimisha siku ya moyo duniani tarehe 29 Septemba tutafanya upimaji katika mikoa wa Arusha, Dar es Salaam na Mwanza. Ninawaomba wananchi mjitokeze kwa wingi kupima afya za mioyo yenu kwani huduma hii tunaitoa bila malipo yoyote yale”, alisisitiza Dkt. Kifai.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Chama cha Wahasibu Wanawake Tanzania (TAWCA) CPA. Tumaini Lawrence aliishukuru Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete kwa huduma ya upimaji na ushauri wa jinsi ya kuepukana na magonjwa ya moyo wanayoitoa kwa wanachama wa chama hicho na kuomba ushirikiano uliopo kati yao uendelee.
“Wanawake wanakabiliwa na majukumu mengi ya kifamilia na mara nyingine hukosa muda wa kupima afya zao, wanaweza kuwa na dalili za ugonjwa fulani lakini wakaona ni sawa na kutokwenda hospitali kwa wakati.Tunaishukuru JKCI kwa huduma mnayoitoa tunaomba mshirikiane nasi ili wanawake wengi zaidi wapate fursa ya kupima na kujua afya zao mapema”.
“Kwa wanachama ambao hawajafanikiwa kupima ninawaomba watenge muda wakapime kwa kuwa afya ya moyo ni kipaumbele cha kila mmoja wetu”, alisema CPA. Tumaini.
Baadhi ya washiriki wa mkutano huo walieleza kufurahishwa na mpangilio mzuri wa utoaji wa huduma na kusema kuwa imewapa uelewa na hamasa ya kuendelea kujali afya zao.
Huduma hiyo ni sehemu ya juhudi za JKCI za kuhamasisha jamii kujikinga na magonjwa ya moyo kupitia upimaji wa mapema, utoaji wa elimu ya afya na ushauri wa kitabibu.