Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhandisi Anthony Sanga, amewasisitiza waajiriwa wapya wa kada ya Mafundi Sanifu na Wapima Ardhi kuhakikisha wanazingatia maadili ya kazi, miiko, taratibu na kanuni zote za utumishi wa umma.
Mhandisi Sanga amezungumza hayo Septemba 19, 2025 jijini Dodoma wakati wa mafunzo ya awali kwa waajiriwa wapya wa Wizara hiyo ikiwa ni sehemu ya kuwajengea uelewa juu ya sheria kanuni, taratibu na miongozo ya utumishi wa umma wakati wanaenda kutekeleza majukumu yao kwenye vituo vya kazi walipopangiwa.
‘’Usimamizi wa maadili ya kazi, kufuata miiko na taratibu ni jukumu linalotakiwa kutekelezwa na kila mfanyakazi, kila mmoja wetu ni sehemu ya Serikali, hivyo ni lazima tuiwakilishe vyema wizara na Serikali kwa ujumla katika maeneo yenu ya kazi” amesema Mhandisi Sanga.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bi Lucy Kabyemera, aliwapongeza waajiriwa wapya kwa kupata nafasi ya kuajiriwa katika wizara hiyo ambapo aliwataka wahakikishe wanawahudumia wananchi kwa kuzingatia sheria pamoja na misingi ya taaluma zao.
“Huduma kwa wananchi ndiyo kiini cha kazi zenu. Hivyo ni muhimu kuzingatia maadili ya kitaaluma ili kuongeza tija kwa Taifa.” Amesema Bi Lucy Kabyemera
Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imepokea watumishi 312 wapya wa kada mbalimbali ambapo mafunzo yaliyofanyika yalihusisha waajiriwa 126 kutoka kada za Mafundi Sanifu na Wapima Ardhi.