Viongozi waandamizi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) wamefanya ziara katika mradi wa Samia Housing II – Kijichi jijini Dar es Salaam, wakilenga kujionea maendeleo ya ujenzi na kujipatia uelewa wa kina kuhusu hatua za utekelezaji wa mradi huo mkubwa wa makazi.
Msimamizi wa Mradi wa makazi ya kisasa wa Samia Housing II – Kijichi Injinia John Edward akitoa maelezo ya maendeleo ya mradi huo kwa Viongozi na wafanyakazi wa NHC.
Ofisa Habari Mkuu wa Mauzo na Masoko wa NHC, Bw. Daniel Kure, akitoa maelezo kwa Viongozi na baadhi ya Maofisa wa Shirika kuhusu maendeleo ya Mradi wa Boulevard.
……
Viongozi wa idara mbalimbali kutoka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) wamefanya ziara ya kikazi kutembelea miradi mikubwa miwili ya ujenzi jijini Dar es Salaam — Samia Housing II, Kijichi na Boulevard Residences, Oysterbay kwa lengo la kujionea maendeleo ya kazi na kupata taarifa za kina kuhusu utekelezaji wa miradi hiyo.
Katika ziara ya Samia Housing II – Kijichi, Msimamizi wa Mradi, Injinia John Edward, aliwapa viongozi hao taarifa kuhusu hatua zilizofikiwa.
Alieleza shughuli mbalimbali za ujenzi zinaendelea kwa kasi na ufanisi, ikiwemo kumwaga zege la awali (blinding) kwa Block E, maandalizi ya hatua za msingi kwa Block D, na uchimbaji wa msingi wa Block A.
Aidha, kazi ya kusafisha mazingira na maandalizi ya eneo la tanki la maji ili kuhakikisha huduma ya maji kwa wakazi wa wa eneo hili inapatikana bila changamoto.
Msanifu Majengo wa mradi huo, Bi. Julieth Prosper, aliwasilisha muundo wa jumla wa mradi na kueleza kuwa awamu ya kwanza inajumuisha majengo matano yenye jumla ya nyumba 100 na awamu ya pili itajumuisha majengo mengine saba, hivyo kufanya idadi kamili ya nyumba kufikia 260.
Kwa upande wake, Afisa Mkuu wa Mauzo na Masoko, Bw. Daniel Kure, alifafanua mikakati ya kibiashara, huku akieleza namna Shirika linavyopanga kuyafikisha makazi hayo sokoni kwa wananchi kwa njia bora na rafiki kwa mteja.
Ziara hiyo pia iliwapa viongozi fursa ya kutembelea mradi wa Boulevard Residences uliopo katika kiwanja namba 105, Oysterbay.
Mradi huo, upo katika hatua za ujenzi, na unatarajiwa kuwa na nyumba 70 zenye viwango vya juu, ambapo 35 zitakuwa kwa ajili ya kupangisha na zingine 35 kwa ajili ya kuuza.
Akizungumza baada ya ziara hiyo, Meneja Mauzo na Masoko wa NHC, Bw. Deogratius Batakanwa, alisema lengo kuu la ziara hiyo ni kuwawezesha viongozi wa Shirika kuelewa kwa undani maendeleo ya miradi, ili wawe mabalozi wazuri kwa umma katika kufikisha taarifa na kuuza makazi hayo.
“Lengo letu ni kuhakikisha Watanzania wanapata makazi bora, salama na yenye huduma zote muhimu. Tunasimamia kila hatua ya mradi kwa umakini ili kuhakikisha unakamilika kwa viwango vya hali ya juu na ndani ya muda uliopangwa,” alisisitiza Bw. Batakanwa.
Naye Meneja Ukusanyaji Madeni wa NHC, Bw. Leviniko Mbilinyi, alipongeza maandalizi ya ziara hiyo na kusisitiza kuwa mikutano ya aina hiyo ni muhimu kwa kuwawezesha viongozi kushuhudia hali halisi ya utekelezaji wa miradi na kutoa mapendekezo ya kuboresha zaidi.
Mradi wa Samia Housing II ni sehemu ya mkakati wa Shirika la Nyumba la Taifa katika kutekeleza dira ya Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuhakikisha kila Mtanzania anapata makazi bora, ya kisasa na yenye huduma za msingi.
Kwa mafanikio haya, NHC inaendelea kujidhihirisha kama nguzo kuu katika sekta ya ujenzi wa makazi nchini, ikichangia kwa vitendo ustawi wa jamii na maendeleo ya taifa.