Askofu Mkuu wa Kanisa la Mungu Anaweza Mshindi Mtawala (MANM), Nabii Evansi Sindano akihubiri katika ibada ya Jumapili iliyofanyika leo Septemba 21, 2025 katika Kanisa la MANM lililopo Tabata Kisukuru, aliyoambatana na maombi maalum ya kuliombea Taifa.
………..
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Askofu Mkuu wa Kanisa la Mungu Anaweza Mshindi Mtawala (MANM), Nabii Evansi Sindano, amewakumbusha Wakristo nchini umuhimu wa kuwathamini na kuwasaidia wazazi wao wakati wote wa maisha yao hapa duniani, kabla ya kutoa sadaka au zaka, kwani wazazi ni chanzo kikuu cha baraka katika maisha ya watoto wao.
Akihubiri katika ibada ya Jumapili iliyofanyika leo Septemba 21, 2025 katika Kanisa la MANM lililopo Tabata Kisukuru, aliyoambatana na maombi maalum ya kuliombea Taifa, Nabii Sindano, amesema kuwa ni lazima kujenga muunganiko wenye matokeo chanya kati ya binadamu na Mungu, pamoja na wale waliowasaidia katika safari ya maisha.
“Ni muhimu sana kuwa na muunganiko sahihi. Tuendelee kumuomba Mungu atupe connection ya kiroho iliyo juu katika maisha yetu. Mungu ndiye Nguvu, naye anaweza – mshindi mtawala,” amesema Nabii Sindano.
Akiendelea na mahubiri yake, Nabii Sindano amewakumbusha waumini wa kanisa hilo kuacha tabia ya kuwasahau watu waliowasaidia wakati wa mapito mbalimbali ya maisha, kwani kuwasahau ni ishara ya kutokujua thamani ya msaada wa kiroho na kijamii walioupata.
Akisoma kutoka katika Kitabu cha Ufunuo 3:19–21, ameeleza kuwa Mwenyezi Mungu hukaa mahali pa juu siku zote, na kwamba licha ya kutufundisha, Yeye huwawazia waja wake mema wakati wote.
Katika ibada hiyo, waumini wa Kanisa la MANM wameliombea Taifa pamoja na familia zao ikiwemo kuondoe roho za mauti na kuleta amani ya kudumu katika nyakati zote.