DAR ES SALAAM, MSANII nyota wa muziki wa Hip Hop, Rosary Robert maarufu kama Rosa Ree, ameanza rasmi maombi na mfungo maalumu wa kuliombea Taifa.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Rosa Ree ameandika ujumbe akieleza kuwa maombi hayo yameanza kwa Sala ya Toba, akisisitiza umuhimu wa mtu kujisafisha kiroho kabla ya kusimama mbele za Mungu.
“Kibinadamu tunafanya mengi ambayo yanatuchafua na kutufanya hatustahili kusimama mbele ya Mungu mtakatifu. Hivyo, kama Musa alivyotakiwa kuvua viatu kabla ya kuzungumza na Mungu kwenye kichaka kilichowaka moto Mlima Horebu (Kutoka 3:5), basi nasi lazima tuvue viatu vyetu vya mizigo yote inayotutia najisi kabla ya kuongea na Mungu,” ameandika Rosa Ree.
Msanii huyo ameendelea kueleza kuwa mioyo ya watu inapaswa kusafishwa kutokana na dhambi mbalimbali za kimwili, kiakili na kiroho, huku akihimiza toba ya dhati inayojenga unyenyekevu mbele za Mungu.
“Tunapotubu lazima tutue mizigo yote, tunyenyekee tukijua sisi hatuna nguvu bila kuwezeshwa na Mungu, na tusalimu amri kwake, Muumba wa mbingu na nchi na mwenye mamlaka yote,” aliongeza.
Kwa mujibu wa Rosa Ree, lengo la mfungo huo ni kumleta Mungu karibu na Taifa na kuamsha mioyo ya watu katika kutafuta utakatifu.
The post Rosa Ree aanza maombi, mfungo wa kuombea Taifa first appeared on SpotiLEO.