Baada ya kuagana rasmi na mabingwa wa kihistoria wa Tanzania, Simba SC, kocha raia wa Afrika Kusini Fadlu Davids sasa amejiunga na wakali wa Morocco, Raja Club Athletic, kama kocha mkuu.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka vyanzo vya karibu na klabu hiyo, makubaliano yote kati ya pande mbili yamekamilika, na Fadlu anarejea katika timu aliyowahi kuitumikia kama kocha msaidizi. Wakati huo, Raja walitwaa ubingwa wa Botola Pro bila kupoteza mchezo wowote msimu mzima, rekodi iliyowaweka kileleni barani Afrika.
Kwa sasa, Davids yupo nchini Afrika Kusini na anatarajiwa kuondoka kesho kuelekea Morocco ili kuanza rasmi majukumu yake. Hatua hii inafungua ukurasa mpya wa maisha yake ya ukocha, safari ambayo safari hii anaingia kama kocha mkuu wa Raja Casablanca.
Raja Club Athletic, moja ya vilabu vikongwe na vyenye mashabiki wengi barani Afrika, imepania kurejea katika nafasi ya juu zaidi, hasa kwenye mashindano ya CAF Champions League. Uongozi wa klabu hiyo umeahidi kumpa Fadlu na benchi lake la ufundi sapoti ya kutosha kuhakikisha ndoto hizo zinatimia.
Kwa ujio wake, mashabiki wa Raja wanatarajia mwendelezo wa falsafa yake ya soka ya kushambulia kwa kasi na nidhamu ya kiufundi, huku wakiamini anaweza kurejea utukufu wa zamani wa klabu hiyo.